Timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, imetwaa ubingwa wa CECAFA U17 baada ya kuichapa Uganda mabao 3-2 kwenye mechi ya fainali iliyochezwa leo Desemba 2, 2025 nchini Ethiopia.
Ushindi huo unaashiria mafanikio makubwa kwa vijana wa Tanzania na pia unawawezesha kufuzu moja kwa moja Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa vijana wa chini ya miaka 17.
Serengeti Boys ilionyesha umahiri mkubwa katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Abebe Bikila nchini Ethiopia, ikitumia mbinu za pamoja, kasi, na uvumilivu kuishinda Uganda yenye historia nzuri katika mashindano ya vijana barani Afrika.
Mabao ya Serengeti Boys kwenye mechi hiyo yamefungwa na Razak Juma Mbegelendi dakika ya sita na 30 na Luqman Mbalasalu dakika ya 45, wakati ya Uganda yamefungwa na Thomas Ogema dakika ya 13 na Brian Olwa dakika ya 90+6.
Mapema katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu, wenyeji Ethiopia waliichapa Kenya mabao 3-0, yaliyofungwa na Dawit Kassaw dakika ya 67, Binyam Abrha dakika ya 79 na Biruk Eyirachew dakika ya 90+3.
Pamoja na kufungwa na Tanzania, Uganda ambao ni mabingwa wa msimu uliopita wanaungana na Serengeti Boys na washindi wa tatu, Ethiopia kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.
Hii itakuwa mara ya nne kwa Serengeti Boys kufuzu AFCON U17 baada ya kufanya hivyo mwaka 2017 mashindano yalipofanyika nchini Gabon, kisha mwaka 2019 Tanzania ikiwa mwenyeji na 2025 nchini Morocco.
