Dar es Salaam. Saa chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kulihutubia Taifa na kubainisha mambo mbalimbali, vyama vya ACT-Wazalendo, Chadema na wanazuoni wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya hotuba hiyo.
Rais Samia ametumia jukwaa la wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhutubia Taifa leo Jumanne, Desemba 2, 2025 akigusia matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025, nafasi ya viongozi wa dini na Tanzania haitakubali kupangiwa ya kufanya na mataifa ya nje.
Msimamo huo wa Rais Samia, unajibu matamko ya wadau mbalimbali liliwemo Bunge la Ulaya, lililoitaka Tanzania kumtoa mahabusu bila masharti Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ili liendelee kuipa misaada Tanzania.
Lakini, kauli hiyo pia inajibu makundi mengine ambayo mara kadhaa katika mitandao ya kijamii, yamekuwa yakitoa masharti ya maridhiano na Serikali, ni kwanza ikubali kuwawajibisha waliohusika na mauaji ya watu siku ya maandamano yaliyozaa vurugu Oktoba 29, mwaka huu.
Mwananchi limezungumza na wadau hao kupata mtazamo wao juu ya hotuba hiyo. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, amesema Taifa linakabiliwa na changamoto kubwa za kisiasa na kijamii, walitarajia Rais achukue nafasi ya kuunganisha Watanzania na kurejesha misingi ya demokrasia na utawala wa haki.
Amesema walitarajia Rais atoke hadharani akiwa kama kiunganishi wa maridhiano na mtu wa kuhimiza haki, lakini badala yake ameonyesha kutokuwa tayari kurejesha misingi hiyo.
“Tunasikitika na kushangazwa kuona Rais hayuko tayari kuonyesha nia njema ya kurudisha Taifa hili kwenye misingi yake ya demokrasia na utu wa kulinda haki za wananchi wake kwanza,” amesema.
Semu amesema ni jambo la kushangaza kwa Rais kuibuka na kulalamikia mabeberu wakati chama chake cha upinzani kilishatoa mapendekezo ya hatua za kuchukua ili kuepusha changamoto zinazoendelea kushuhudiwa sasa.
“Tunavyoona anakoelekea, Rais haendi kusuluhisha kwa sababu hataki kukubali hadharani makosa ya viongozi wake na chama chake. Bila hatua hiyo, hakuna mchakato wa kweli wa kuponya Taifa na kupata suluhu ya haki,” amesema.
Kwa mujibu wa Semu, Serikali imeendelea kudharau na kubeza hoja pamoja na mapendekezo ya vyama vya upinzani ambavyo hupitishwa kwenye changamoto lukuki na chama tawala chenyewe.
“Vyama vya upinzani tumesema mengi. Tulipendekeza mambo ya msingi lakini tukadharauliwa. Tumeona uonevu dhidi ya wagombea wetu wa urais, ubunge na udiwani walienguliwa bila sababu za msingi yote haya yalifanyika hadharani, si kwa siri,” amesema.
Akizungumzia hoja ya Rais ya maridhiano, Semu amesema ACT-Wazalendo kilishiriki mchakato huo tangu mwaka 2021, lakini baadaye wakatambua kuwa zilikuwa hadaa zisizo na dhamira njema.
“Tuligundua chama na Serikali yake hawakuwa na nia ya kweli ya kuleta mabadiliko. Tumeona namna chaguzi za serikali za mitaa zilivyoendeshwa nguvu zilitumika, haki za wananchi zikiporwa. Na tunaona katika uchaguzi mkuu wa 2025,” amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Rugemeleza Nshala, amesema kauli ya Rais Samia kuhusu matumizi ya nguvu inaashiria kuhusika kwa vyombo vya dola katika matukio ya mauaji yaliyoripotiwa wakati wa machafuko.
“Kama kweli vyombo vya dola vilitumia nguvu inayopaswa kukabiliana na waandamanaji, basi shetani alikuwa kazini. Inathibitisha walikuwa nyuma ya mauaji,” amesema Dk Nshala.
Kuhusu uamuzi wa Chadema kususia uchaguzi, Dk Nshala amesema hata kama chama hicho kingeshiriki, matokeo yasingebadilika kwa kuwa walikataa kile alichokiita hila za chama tawala.
“Aliona vituo ambavyo kura zilikuwa zinahesabiwa, ule haukuwa uchaguzi bali ulikuwa ni udanganyifu. Chadema ilijua kinachofanyika ni udanganyifu. Tulikataa kubariki udanganyifu huo,” amesema.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa, Dk Sabato Nyamsenda amesema kulingana na hali inayopitia nchi imegawanyika vipande na matarajio ya wadau wengi hotuba yake ilipaswa kuja kuunganisha nchi bahati mbaya haijajibu kiu ya wengi.
Nyamisenda amesema hotuba yake imekuwa na ‘narative’ nyingi na haiwezi kutibu majeraha isipokuwa mgawanyiko utaendelea.
“Kama Serikali imejiridhisha na inafahamu chanzo cha haya matukio kulikuwa hakuna haja ya kuunda tume, kwa kauli yake kuna namna inaenda kubinya uhuru wa tume kutekeleza majukumu yake,”amesema.
Pia amesema hata kama tume hiyo itashangaza kwa kuja na uchunguzi wa kuridhisha wengi kinyume na matarajio, bado Serikali haitakuwa tayari kuyatekeleza ili kuondoa mkwamo.
Kwa upande wake, Mwanadiplomasia mwandamizi, Balozi Benson Bana amesema uamuzi wa Rais Samia kuzungumza na Taifa kupitia Baraza la Wazee wa Dar es Salaam umekuja kwa wakati muafaka, akisema hatua hiyo inadhihirisha nafasi yake kama kiunganishi na mshikamano wa Watanzania.
Akimnukuu Rais Samia, Balozi Bana amesema tukio la Oktoba 29 na matukio yaliyoendelea baadaye si sehemu ya utamaduni wala mila za Watanzania, na yeyote mwenye mapenzi mema na nchi anatakiwa kulilaani na kumuomba Mungu lisijirudie.
Bana amesema kilichojitokeza kilikuwa ni jaribio la kuchokoza dola kwa lengo la kuidhoofisha au kuiondoa madarakani kinyume na Katiba, jambo ambalo liliibua vurugu zisizo na tija kwa Taifa.
Balozi Bana amesema hotuba ya Rais imebeba maonyo, busara na uelekeo sahihi wa kitaifa, ikiwemo wito kwa wenye malalamiko kutumia njia halali kuwasilisha madai yao, akisisitiza kuwa uongozi wa taifa lolote hupangwa na Mungu.
Amebainisha maudhui ya hotuba hiyo yamejikita kwenye falsafa ya 4R ya Rais Samia, akiwataka Watanzania kumuunga mkono kiongozi wao na kufuata sheria katika kudai haki.
Kuhusu siasa za ushindani, Bana amesema vyama vya upinzani vina wajibu wa kushiriki uchaguzi, kushindana kwa hoja, na kuwashawishi wananchi, badala ya kuvuruga amani ya Taifa.
“Dola lazima ilindwe. Vyombo vya usalama vipo kulinda mamlaka, wananchi na mali za Watanzania. Ukivuruga, wanakuvuruga. Hotuba yake imekuja wakati muafaka na wengi walikuwa wakiitamani,” amesema.
Amesema ujumbe wa Rais umewafikia Watanzania wote na ni wito wa kutafakari, kuheshimiana, na kuliweka Taifa mbele ya masilahi binafsi.
