Mgombea urais wa Chama cha National Unity Platform (NUP), Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine amewataka wafuasi wake na wananchi katika Wilaya ya Luweero nchini Uganda kuwachagua viongozi wapya ili kuhakikisha wanaiondoa Serikali ya Chama cha National Resistance Movement inayoongozwa na Rais Yoweri Museveni.
Kiongozi huyo ameapa kuiondoa Serikali iliyopo madarakani, ambayo anaituhumu kupuuza tatizo la uporaji ardhi. Amesema Serikali ya NRM haijali wananchi wanaolalamikia kunyang’anywa ardhi yao katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo Luweero.
“Kuendelea kuwepo madarakani NRM ni sawa wananchi wetu kuendelea kupoteza ardhi kwa wanyang’anyi, pia ni sawa watu wetu kukosa huduma nyingine muhimu. Lakini nawaambia kwamba hii siyo sawa. Tutarejesha ardhi yetu tutakapoiangusha NRM ifikapo Januari 15, 2026,” amesema.
Bobi Wine amewaambia wafuasi wake kuwa kampeni zinazoendelea ni harakati za kuiokoa Uganda kutoka kwenye mfumo uliozorotesha sekta zote za uchumi.
“Kama hizi zingekuwa kampeni za kawaida, chama tawala na mfumo wake wasingekuwa wakitumia mabilioni ya shilingi kujaribu kumzuia Bobi Wine kufanya kampeni. Mmeona wanajeshi na polisi wanaojaa barabara kuu na kukwamisha harakati zangu, hasa katika eneo la Buganda,” amesema.
Mwanasiasa huyo mwenye ushawishi nchini humo, amefanya mikutano ya kampeni katika Halmashauri ya Mji ya Zirobwe na Parokia ya Kyegombwa katika Halmashauri ya Mji ya Luweero na kuwaeleza kuwa serikali ya NRM imelenga kampeni zake katika eneo la Buganda kwa kuzuia wapinzani, kuwatawanya kwa gesi ya machozi wafuasi wake.
“Hata tunapozungumza sasa, mmoja wa wafuasi wetu amefariki kutokana na majeraha. Hivi ndivyo tunavyopitia katika kampeni hizi,” amesema.
Kwa mujibu wa Mtandao wa The Monitor, halikuweza kuthibitisha taarifa ya kiongozi huyo wa upinzani kuhusu mfuasi huyo anayedaiwa alifariki dunia jana.
Mkazi wa Kata ya Nyimbwa wilayani Luweero, Amina Nankinga amesema amepoteza ekari tatu kwa watu kwa wanyang’anyi wa ardhi.
“Hatujapata bado ulinzi dhidi ya watu wanaochukua ardhi yetu. Nataka Rais ajaye ahakikishe wamiliki maeneo wanapata usalama wa ardhi yao. Wanyang’anyi wa ardhi ni watu wenye nguvu sana,” amesema.