Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, ametangaza kikosi cha awali cha wachezaji 53 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, uteuzi ambao hapana shaka utawaweka katika presha kubwa nyota wa baadhi ya nafasi.
Wachezaji hao 53, watapaswa kupunguzwa hadi kubakia 28 ambao wanahitajika katika orodha ya mwisho ya Fainali hizo, jambo ambalo linatoa ishara kuwa siku 10 za maandalizi kabla ya kikosi cha mwisho kutangazwa zitakuwa na ushindani mkubwa baina ya nyota hao.
Ushindani mkubwa unaonekana utakuwa katika nafasi ya beki wa kulia ambayo Kocha Gamondi amewaita Shomari Kapombe wa Simba, Lusajo Mwaikenda (Azam FC), Haji Mnoga (Salford City), Israel Mwenda (Yanga) na Miano Danilo (Paneveys).
Kama Gamondi ataamua kwenda AFCON na makipa wanne, hakutakuwa na presha katika eneo hilo ingawa akiamua kuwatumia makipa watatu, ugumu utakuwa zaidi kwa Yona Amos na Zuberi Foba kuwania nafasi moja itakayobakia kati ya tatu, kwa vile Hussein Masalanga na Yakoub Suleiman wamekuwa na muendelezo wa kuitwa kikosini na hata kupata fursa ya kucheza.
Dickson Job, Ibrahim Abdulla na Wilson Nangu hawaonekani kuwa katika presha kubwa kwenye nafasi ya beki wa kati kama itaavyokuwa kwa Mukrim Abdallah, Elias Lawi, Vedastus Masinde, Bakari Mwamnyeto, na Abdulmarik Zakaria.
Idadi kubwa ya wachezaji walioitwa katika nafasi ya kiungo na ile ya ushambuliaji, inaonyesha wazi kutakuwa na ushindani mkubwa wa nyota wa nafasi hizo kuwania uwepo wao katika fainali za AFCON baadaye mwaka huu.
Wachezaji 53 wanaounda kikosi cha awali cha Taifa Stars ni Hussein Masalanga, Yakoub Suleiman, Yona Amosi, Zuberi Foba, Haji Mnoga, Iddi Selemani, Ibrahim Abdullah, Dickson Job, Feisal Salum, Cyprian Kachwele, Ahmed Pipino, Abdul Suleiman na Mbwana Samatta.
Wengine ni Morice Abraham, Pascal Msindo, Wilson Nangu, Mohamed Hussein, Lusajo Mwaikenda, Mukrim Abdallah, Nassor Saadun, Elias Lawi, Yusuph Kagoma, Shomari Kapombe, Mudathir Yahya, Saimon Msuva, Athuman Makambo, Vedastus Masinde, Bakari Mwamnyeto, Novatus Miroshi, Tarryn Allarakhia, Charles M’mombwa, Iddi Kipagwile, Vitalis Mayanga, Khalid Habibu na Edwin Balua.
Pia kuna Miano Danilo, Alphonce Mabula, Nathaniel Chilambo, Said Khamis, Suleiman Mwalimu, Yahya Zaydi, Offen Chikola, Jackson Kasanzu, Kibu Denis, Israel Mwenda, Kelvin John, Sabri Kondo, Nickson Kibabage, Paul Peter na Abel Josiah.
Katika Fainali za AFCON 2025 zitakazofanyika Morocco, Taifa Stars imepangwa kundi C na timu za Tunisia, Nigeria na Uganda.