MASHUJAA imetoka sare ya pili mfululizo katika mechi za Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji na Coastal Union na kukata wimbi la ushindi kwa timu hiyo na kocha Salum Mayanga amefichua kilichowaponza kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma.
Timu hiyo imecheza mechi nne mfululizo na kushinda mbili dhidi ya Namungo na Mbeya City ilizozifunga bao 1-0, kisha kubanwa na Dodoma Jiji na juzi mbele ya Coastal Union na kocha Mayanga aliliambia Mwanaspoti kucheza mechi mfululizo kulikomfanya abadili kikosi ni sababu.
Mayanga alisema ilimlazimu kubadilisha kikosi katika mechi mbili zilizopita ili kuwapa nafuu wachezaji, kityu kilichowapunguzia kasi ya wimbi la ushindi walilokuwa nalo hivi karibuni kwani wale waliopewa nafasi walishindwa kufanya kile alichokitarajia.
“Ni kweli mechi mbili tumeshindwa kufunga bao hata moja nafikili ni nidhamu ndogo ya kutumia nafasi kwa wachezaji wangui kwani walifanijkiwa kutengeneza nafasi nyingi lakini walishindwa kuzitumia,” alisema Mayanga na kuongeza;
“Ukiondoa hilo pia safu yangu ya ulinzi licha ya kuto kuruhusu mabao kwenye mechi nne mfululizo wameonyesha udhaifu mkubwa nawapongeza hawakuruhusu mabao lakini kuna kazi kubwa imefanywa na kipa.”
Mayanga alisema amerudi kwenye uwanja wa mazoezi na kikosi chake kuna mambo muhimu ya kuyafanyia kazi kabla ya kurudi tena kusaka nafasi ya kufanya vizuri ili waweze kuendana na kasi ya ligi kuu huku akiweka wazi kuwa huu ni msimu mgumu zaidi.
“Tumekuwa na mechi mfululizo ili kuweka usawa kwa wachezaji wangu kukwepa majeruhi ya lazima niliamua kufanya mabadiliko ya kikosi kulingana na mpinzani lakini hakujawa na muendelezo mzuri nafikiri sababu ni wachezaji niliowapa nafasib kutokuwa na utimamu mzuri nashukuru hawakudondosha pointi zote tatu.”