Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini limebainisha mambo 12 linayodai yanaendelea kupangwa mitandaoni kuelekea Desemba 9, 2025, huku likiwaonya wanaopanga na kuhamasisha vitendo vya uvunjifu wa amani siku hiyo kuachana navyo, la sivyo watashughulikiwa.
Polisi wamebainisha hayo siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kulihutubia taifa na kueleza jinsi Serikali ilivyojipanga wakati wote kudhibiti vitendo vya kihalifu.
Rais Samia alitoa kauli hiyo kufuatia kilichotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025 yalipofanyika maandamano yaliyozaa vurugu katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Mara, Mbeya, Geita, Dodoma na Arusha.
Vurugu hizo zilisababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa mali za umma na binafsi. Miongoni mwa mali zilizoathirika zaidi ni kuchomwa moto vituo vya polisi, ofisi za serikali za mitaa, vituo vya mafuta na mabasi yaendayo haraka na nyumba za watu kadhaa.
Jana Desemba 2, 2025, Rais Samia akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaa, alisema kilichokuwa kimepangwa ni kuiangusha Serikiali yake, akisisitiza akiwa mkuu wa nchi ameapa kuilinda Tanzania na kuwaonya wanaopanga njama za Desemba 9 au 25, kwamba wamejipanga wakati wowote kuzuia uvunjifu wa amani.
Leo Jumatano Desemba 3, 2025, Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa umma kuhusu kile lilichoita njama zinazoratibiwa kupitia mitandao ya kijamii na makundi mbalimbali ya sogozi, zenye lengo la kuvuruga amani nchini.
Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamanda David Misime, imesema kumekuwepo na mfululizo wa ujumbe katika mitandao ya kijamii unaohamasisha vitendo 12 vinavyoashiria uvunjifu wa amani, ikiwemo kuzuia shughuli za kiuchumi na kuvuruga miundombinu muhimu ya mawasiliano.
Misime ameeleza kuwa ujumbe huo, unaohamasishwa kupitia mitandao na makundi sogozi, unatumiwa kuwahamasisha watu kufanya maandamano yasiyo na kikomo kuanzia Desemba 9, huku baadhi ya wachochezi wakitoa maelekezo kuhusu matumizi ya silaha.
“Wameelekezana kwamba asiyejua kutumia silaha awaachie waliopata mafunzo ya matumizi ya silaha. Hii maana yake ni kwamba watu hawa wanazo silaha za kutimiza makusudio yao,” amesema Misime.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, baadhi ya ujumbe unaohamasishwa unawahimiza watu kuchoma na kuharibu minara ya mawasiliano ili nchi ikose huduma, kufunga barabara zinazotoka na kuingia bandarini, na kuziba mipaka yote ya kuingia na kutoka nchini.
Aidha, Misime alisema kuwa taarifa zilizopo zinaonyesha kuwepo kwa mpango wa kuvamia hospitali na kuzuia utoaji wa huduma, pamoja na kuwalenga watumishi wa Serikali kwa madhara binafsi.
“Wamefikia hatua ya kusema kuwa watakaoandamana siku hiyo watakutana na watu waliokatana vichwa mitaani. Wengine wameapa kutowaruhusu waandamanaji kufika katika maeneo yao,” alisema.
Jeshi la Polisi pia limekumbusha madhara ya vurugu za Oktoba 29, 2025, zilizosababisha vifo vya watu na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya Serikali na binafsi, ikiwemo vituo vya polisi, vituo vya mafuta na magari kuchomwa moto.
Misime amesema baadhi ya wananchi wametoa kauli za kutokubali kuona hasara kama ile ikijirudia, na hivyo kujipanga “kulinda maisha, familia na mali zao kuanzia Desemba 9 na kuendelea.”
Amesema kampeni za kuchochea maandamano yasiyo na kikomo haziwezi kuitwa haki, kwa kuwa zinavunja haki za watu wengine wanaotegemea shughuli za kila siku kujipatia riziki.
“Huu ni uhalifu mkubwa unaoendelea kuhamasishwa. Kwa nchi yoyote duniani, hali kama hii ni tishio kubwa kwa maisha ya watu, uchumi wa taifa na ustawi wa kijamii,” amesema Misime.
Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuwa makini na kukataa kushiriki au kuunga mkono watu wanaohamasisha uvunjifu wa amani, likisisitiza kuwa malengo ya makundi hayo ni kulirudisha taifa kwenye machungu yaliyoshuhudiwa mwezi uliopita.
Katika hatua nyingine, Polisi imewasihi wananchi kuendelea na maandalizi ya sikukuu za mwisho wa mwaka kwa kuzingatia usalama wa maisha na mali zao.
“Jeshi la Polisi linaendelea kutoa wito kwa wananchi wote kwa nafasi zao kuanzia ngazi za familia kuwakataa watu kama hawa pamoja na wanayoyahamasisha. Malengo yao ni kuharibu Taifa letu na kuturudisha kwenye machungu na madhara yalitokea Oktoba 29,” amesema.
Limewashauri watakaosafiri waachae waangalizi au walinzi katika makazi yao, vilevile wazingatie sheria za usalama barabarani na ishara mbalimbali zilizopo ili kuepuka ajali.
Kufuatia taarifa hiyo, Ofisa mwandamizi mstaafu wa Jeshi la Polisi, Jamal Rwambow amewataka Watanzania kuzingatia maelezo yaliyotolewa na Rais Samia, aliyesema Serikali haiwezi kuruhusu watu au kikundi cha watu kuharibu usalama wa nchi.
Katika mazungumzo yake na Mwananchi, Rwambow aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi Kinondoni, amesema: “Nisisitize tu, tujiepushe na tuwakanye vijana na watoto wetu wasijiingie kwenye mambo ya vurugu, ili tusije tukapata madhara kama yaliyotokea Oktoba 29. Tahadhari ya polisi si ya kupuuzia, izingatiwe.”
“Tuzidi kuwaonya vijana wetu, lakini kupitia maridhiano basi wapate nafasi katika Tume ya Jaji Chande (Othman) kueleza yale yanayowasibu. Lakini inasikitisha hizi vurugu hazipaswi kupuuziwa kwa sababu zinatuchafua sana, tukiendelea kujifachafua haitapendeza,” amesema Rwambow.
Hata hivyo, Rwambow alikuwa na mtizamano tofauti kidogo kuhusu polisi kutoa taarifa hiyo, akisema hazipaswi kuwa wazi kwa sababu yakitokea ya kutokea wananchi wanalinganisha matukio hayo na kilichosemwa katika taarifa ya jeshi hilo.
Aidha, Rwambow amesema haiondoi ukweli kwamba polisi wamejiandaa vizuri na atakayebainika kuvuruga asiilaumu Serikali kwa yatakayotokea.
“Hatutakuwa tayari wale wanaokwenda kwa sura ya maandamano, lakini wanakwenda kukwamisha shughuli za bandari ili kuharibu uchumi wetu unaotegemea bandari.
“Vyombo vya vyote vya ulinzi na usalama vina kila sababu ya kuchukua hatua kali zaidi ili kuhakikisha uharibifu huo hautokea tena. Haifai kuijaribu Serikali kwa njia yoyote, hawa vijana wanaogizwa fanya hili au lile ni kujitafuta matatizo,” ameeleza.
