Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amewataka watendaji wa Wizara ya elimu kusimamia nidhamu na uwajibikaji ili kutekeleza kikamilifu mipango ya wizara
Hemed ameyasema hayo katika kikao maalumu cha viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, kilichofanyika leo Desemba 3, 2025 katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi.
Amesema mafanikio ya wizara hayawezi kupatikana bila viongozi kuhakikisha walimu na watumishi wengine wanafanya kazi kwa kuzingatia wajibu wao. Aidha, amekumbusha umuhimu wa matumizi sahihi ya fedha na usimamizi wa mali za serikali ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vinavyostahili.
Hemed amewataka wakurugenzi kufanya ufuatiliaji wa karibu katika maeneo yao ili kubaini changamoto zinazojitokeza na kutoa ufumbuzi wa haraka. Pia ameielekeza wizara kuharakisha uundwaji wa Tume ya Utumishi wa Walimu itakayoshughulikia masilahi na nidhamu za walimu.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Lela Mohamed Mussa ameishukuru Serikali ya awamu ya nane kwa kuipa sekta ya elimu kipaumbele kuanzia maandalizi hadi elimu ya juu, na ameahidi kuwa viongozi na watendaji wa wizara wapo tayari kutekeleza maagizo yote yanayolenga kuboresha elimu nchini.