Dar es Salaam. Tanzania imetajwa miongoni mwa vinara barani Afrika katika kupambana na usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, ikiwa imepiga hatua katika miaka michache iliyopita na kuvutia kutambuliwa kimataifa.
Hatua hizi zimebainishwa wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya saba ya Wiki ya Uelewa wa Usugu wa Dawa Afrika, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi wa afya wameipongeza Tanzania kwa mafanikio yaliyotokana na uwekezaji wa kisera, kiutendaji na kiutafiti.
Akizindua maadhimisho hayo leo Desemba 3, 2025, Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi alisema Tanzania imetekeleza kwa mafanikio Mpango wa Pili wa Kitaifa wa Kupambana na usugu wa dawa (AMR) – 2023–2028 kwa mtazamo wa One Health, unaounganisha sekta za afya ya binadamu, mifugo, kilimo na mazingira.
Alisema utekelezaji huo umewezesha kupungua kwa vifo vinavyohusishwa na AMR kwa asilimia 14 na kupunguza matumizi ya dawa za kuua vimelea (viuavijasumu) nchini kwa zaidi ya asilimia 80.
Wakati Dk Nchimbi akitaja mafanikio hayo, Novemba 30, 2025 wakitoa mafunzo kwa wanahabari, wataalamu wa afya walisema tatizo la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa (Uvida) linazidi kukua nchini, ambapo takwimu zinaonyesha mwaka 2021 lilisababisha vifo vya watu 42,196.
Lakini katika hotuba yake, Dk Nchimbi alisema: “Zaidi ya hapo, Tanzania imeongeza ufadhili wa ndani kwa shughuli za AMR na kuimarisha uwazi kwa kushiriki takwimu kwenye majukwaa ya kikanda na kimataifa,” amesema Dk Nchimbi.
Katika upande wa uelimishaji, Dk Nchimbi aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, alisema nchi imepiga hatua, lakini:
“Kampeni ya ‘holelaholela itakukosti’ ambayo imewafikia watu karibu milioni 25, imetambuliwa na Africa CDC kama mfano bora wa ubunifu, unaounganisha sayansi na sanaa katika utoaji elimu ya afya,” alisema.
Dk Nchimbi alisema sekta ya afya imeimarika kupitia maboresho ya mifumo ya kudhibiti maambukizi (IPC) na Afya ya Maji, Usafi na Mazingira (WASH), hatua zilizosaidia kufikia ongezeko la asilimia 60 katika uzingatiaji wa miongozo ya kudhibiti maambukizi.
Ametaja mafanikio mengine ni pamoja na mfumo madhubuti wa usambazaji wa dawa kupitia Bohari ya Dawa (MSD), udhibiti wa ubora na usalama wa dawa kupitia TMDA, pamoja na utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za afya zilizo bora kwa wananchi wote bila ubaguzi.
“Kwa hatua hizi, Tanzania imepanda kutoka kiwango cha chini (Level 1) mwaka 2016 hadi viwango vya juu vilivyokomaa (Levels 3 na 4) mwaka 2024 katika tathmini ya kimataifa ya utekelezaji wa mikakati ya AMR.
Mafanikio haya yanaiweka nchi katika nafasi ya kipekee barani Afrika, ikionekana kuwa mfano kwa mataifa mengine katika kupambana na tishio la usugu wa dawa duniani,” amesema Dk Nchimbi.
Amewataka Watanzania na nchi wanachama wa Afrika kutumia dawa kwa uangalifu, kuzingatia ushauri wa kitaalamu, na kuendelea kushirikiana ili kulinda ufanisi wa dawa na afya za vizazi vijavyo.
Janga linalosonga polepole
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni janga linalosonga polepole, lisiloambatana na ving’ora, linatambaa kimyakimya, likirudisha nyuma maendeleo ya tiba na kutishia afya ya binadamu, ustawi wa wanyama, usalama wa chakula na mazingira.
“Wajibu uko mikononi mwa kila mmoja wetu madaktari, wafamasia, wanasayansi wa maabara, madaktari wa mifugo, watendaji wa mazingira, watunga sera, wakulima na jamii kwa ujumla,” alisema.
Mchengerwa amesema AMR haiwezi kuanzia tu maabara, inaanzia majumbani, mashambani, madukani kwa wafamasia na katika tabia za kila siku.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Edwin Mhede amesema katika sekta ya mifugo wameendelea kuboresha biosecurity na kampeni za chanjo, kupunguza maambukizi kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, huku ukaguzi wa mara kwa mara wa bidhaa za mifugo ukiboresha usalama wa chakula.
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi amesema wataalamu wa afya wamekuwa wakiahirisha upasuaji kwa sababu mteja ameshindwa kuponywa na dawa na familia inalipia matibabu lakini mgonjwa anafariki kwa sababu ya usugu wa dawa.
Amesema iwapo hali hiyo haitaweza kuzuilika, itaua watu wengi zaidi miaka ijayo na ni janga linalowaingiza wengi katika umasikini.