MKURUGENZI wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Ayub Rioba Chacha, amesema mechi 32 za kuwania Fainali ya Mataifa ya Afrika (AFCON) zitarushwa mubashara bure kwenye chaneli ya TBC1 na TBC Taifa kwa ubora na ubunifu.
Fainali hizo zitakazofanyika nchini Morocco kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026, timu ya taifa ya Tanzania itashiriki ikiwa ni mara ya nne baada ya 1980, 2019, 2023 na sasa 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za TBC zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam leo Desemba 4, 2025, Rioba amesema kama ilivyo utamaduni wa TBC, watakikisha Watanzania wanapata matangazo ya moja kwa moja ya mechi mbalimbali za michuano hiyo mikubwa barani Afrika bila malipo.
Ameongeza kuwa, TBC imepata haki ya kurusha jumla ya mechi 32 kati ya 52, kulingana na mpangilio uliowekwa na waandaaji wa michuano hiyo.
Pia amesistiza mechi hizo hazitaathiri vipindi vingine, hivyo wataweka mpangilio mzuri wa kuhakikisha kila Mtanzania anafurahia akipendacho kwenye chaneli hizo.
“Ndugu Waandishi wa Habari kama ilivyo utamaduni wa TBC tutarusha matangazo mubashara bure kwa lugha ya Kiswahili kupitia TBC1 na TBC Taifa, kama tujuavyo michuano hiyo ni tamasha linalokutanisha tamaduni mbalimbali za Kiafrika kuanzia vyakula, mavazi na hata kelele za uwanjani,” amesema Rioba na kuongeza.
“Hivyo kwa kuunga mkono matukio hayo, TBC itahakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kufuatilia mechi za timu zao pendwa kwa ubora wa hali ya juu, hivyo Watanzania wafahamu kuwa tuko tayari kuwapa uhondo wote.”
Katika fainali hizo zitakazoshirikisha mataifa 24 yaliyofuzu, Taifa Stars imepangwa kundi C na timu za Nigeria, Tunisia na Uganda.
Desemba 23, 2025, Taifa Stars itaanza kucheza dhidi ya Nigeria, kisha itaikabili Uganda (Desemba 27, 2025), itamaliza hatua ya makundi Desemba 30, 2025 dhidi ya Tunisia.
