Siku 61 za Pantev na mastaa wanne tu Simba

KOCHA Dimitar Pantev aliyekuwa akitambulishwa kama meneja mkuu wa Simba amehitimisha siku 61 na huwezi kuamini siku hizo kuna mastaa wanne pekee waliotumika zaidi katika kikosi hicho chenye wachezaji 27, huku akizungumza na Mwanaspoti.

Pantev aliyetambulishwa Oktoba 3 kama meneja mwenye taaluma ya ukocha, ameiongoza Simba katika mechi tano za mashindano ikiwamo moja ya Ligi Kuu Bara (1) na nne za Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya juzi kusitishiwa mkataba. Kutoka Oktoba 3, 2025 hadi Desemba 2, 2025, ni siku 61 zilizohitimisha maisha ya Mbulgaria huyo Simba baada ya uongozi wa klabu hiyo kusitisha mkataba kwa makubaliano ya pande mbili.

Katika mechi hizo tano, wachezaji wanne ambao hawajawahi kukosa kuanza kikosi cha kwanza nao ni kipa Yakoub Suleiman, beki wa kushoto Antony Mligo, beki wa kati Rushine De Reuck na winga Joshua Mutale.

Wakati hao wakiwa panga pangua, pia kuna wenginesaba hawakupata nafasi ya kucheza chini ya Pantev kwa sababu mbalimbali wakiwemo majeruhi kama Moussa Camara, Mohamed Bajaber na Abdulrazak Hamza. Pia kuna Charles Semfuko, Mzamiru Yassin na kipa Hussein Abel walioishia benchi, wakati Vedastus Masinde hakuonekana kabisa.

Mengi yamezungumzwa kwa kusitishwa mkataba wa Pantev, ikiwamo ishu  ya upangaji wa kikosi uliokuwa hauwaridhishi viongozi na hata wachezaji wa timu hiyo.

Pantev kuna wakati alikuwa hatumii mshambuliaji asilia, huku katika mechi hizo tano, alikuwa akifanya mabadiliko ya wachezaji hadi kufikia watano kila mechi, ikidhihirisha aliokuwa akijitafuta katika kuunda kikosi kazi cha ushindi, kabla hajatumuliwa mara alipotua akitokea Bamako, Mali.

Kama hujui hadi anaondoka Simba, Pantev ametumia jumla ya wachezaji 21, lakini ni wawili pekee ndio waliomaliza dakika 90 za kila mechi ambao ni Yakoub Suleiman na Antony Mligo waliotumika kwa dakika 450 kila mmoja.

Mutale aliyecheza mechi zote tano akianza kikosi cha kwanza, hakuwahi kumaliza dakika 90 hata mara moja, huku Rushine ni mechi moja pekee aliishia dakika 45 za kwanza, zingine akimaliza 90. Mchezaji aliyetumika kwa dakika chache zaidi ukiachwa wale ambao hawajatumika kabisa ni Awesu Awesu aliyecheza kwa dakika tatu. Akifuatiwa na Ladack Chasambi (dk 17) na David Kameta (dk 90).

Takwimu za jumla zipo hivi; Yakoub Suleiman (dk 450), Antony Mligo (dk 450), Rushine (dk 405), Shomari Kapombe (dk 360), Elie Mpanzu (dk 357), Wilson Nangu (dk 345), Joshua Mutale (dk 311), Naby Camara (dk 323), Neo Maema (dk 280), Jean Charles Ahoua (dk 236). Wengine ni Morice Abraham (dk 230), Alassane Kante (dk 183), Jonathan Sowah (dk 169), Kibu Denis (dk 150), Chamou Karaboue (dk 150), Yusuf Kagoma (dk 142), Steven Mukwala (dk 124), Selemani Mwalimu (dk 113), David Kameta (dk 90), Ladack Chasambi (dk 17) na Awesu (dk 3).

Katika mechi tano za Pantev, imeshinda mbili, sare moja na kupoteza mbili. Timu imefunga mabao sita, yenye ikifungwa manne na waliofunga mabao ya Msimbazi ni; Wilson Nangu (2), Kibu Denis (2), Jonathan Sowah (1) na Neo Maema (1).

Ilikuwa mechi ya kwanza iliyochezwa Oktoba 19, 2025 ikiwa ni raundi ya pili Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba kushinda 3-0, yakifungwa na Wilson Nangu na Kibu Denis aliyepachika mawili.

Simba ikiwa ugenini, kikosi kilichoanza kilikuwa na mabadiliko ya wachezaji wanne kutoka kile kilichoichapa Namungo 3-0, benchi la ufundi liliongozwa na Seleman Matola.

Jean Charles Ahoua, Wilson Nangu, Neo Maema na Seleman Mwalimu, walianza dhidi ya Nsingizini, badala ya Chamou Karaboue, Morice Abraham, Yusuf Kagoma na Steven Mukwala walioanza dhidi ya Namungo.

Kikosi dhidi ya Nsingizini kilikuwa hivi; Yakoub Suleiman, Antony Mligo, Joshua Mutale, Jean Charles Ahoua, Shomari Kapombe, Rushine De Reuck, Naby Camara, Wilson Nangu, Elie Mpanzu, Neo Maema na Selemani Mwalimu.

Benchi kulikuwa na Hussein Abel, David Kameta, Chamou Karaboue, Yusuf Kagoma, Ladack Chasambi, Jonathan Sowah, Steven Mukwala, Morice Abraham na Kibu Denis.

Wachezaji waliotokea benchi ni Chamou, Kagoma, Sowah, Kibu na Morice waliochukua nafasi za Mutale, Ahoua, Nangu, Mwalimu na Maema.

Marudiano ya mechi hiyo ilikuwa Oktoba 26, 2025, suluhu ikaihakikishia Simba kufuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa ikipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Pantev alibadilisha wachezaji watano kutoka kikosi kilichocheza ugenini. Walioingia kikosini ni Chamou Karaboue, Morice Abraham, Yusuf Kagoma na Kibu Denis ambao awali walitokea benchi. Pia David Kameta ‘Duchu’ alicheza kwa mara ya kwanza.

Kikosi kilikuwa hivi; Yakoub Suleiman, Chamou Karaboue, Antony Mligo, Joshua Mutale, Jean Charles Ahoua, David Kameta, Morice Abraham, Yusuf Kagoma, Rushine De Reuck, Elie Mpanzu na Kibu Denis.

Benchi walikuwepo Hussein Abel, Shomari Kapombe, Wilson Nangu, Naby Camara, Awesu Awesu, Alassane Kante, Neo Mema, Jonathan Sowah na Steven Mukwala. Kipindi cha pili, Awesu, Kante, Maema, Sowah na Mukwala waliingia kuchukua nafasi za Mutale, Ahoua, Morice, Kagoma na Mpanzu.

Hii ilikuwa mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa Novemba 8 Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na Nangu na Sowah waliifungia Simba mabao hayo baada ya Edward Songo kuitanguliza JKT.

Kikosi kilichoanza, pia kilikuwa na mabadiliko ya nyota watano tofauti na kile kilichocheza dhidi ya Nsingizini. Kapombe, Nangu, Kagoma, Camara na Maema walianza, badala ya Chamou, Duchu, Morice, Ahoua na Mpanzu.

Kikosi kilikuwa hivi; Yakoub Suleiman, Shomari Kapombe, Antony Mligo, Wilson Nangu, Rushine De Reuck, Yusuf Kagoma, Kibu Denis, Naby Camara, Steven Mukwala, Neo Maema na Joshua Mutale.

Waliokuja kuingia baadaye ni Alassane Kante, Mpanzu, Sowah, Ahoua na Morice. Walichukua nafasi za Kagoma, Kibu, Mukwala, Maema na Mutale.

Novemba 23, Simba ilianza makundi Ligi ya Mabingwa kwa kipigo cha nyumbani bao 1-0. Pantev kama kawaida, alifanya mabadiliko kidogo ya kikosi wachezaji watatu kutoka kile cha mwisho kilichoshinda mechi ya ligi dhidi ya JKT Tanzania. Kante, Morice na Mpanzu walianza, badala ya Kagoma, Kibu na Mukwala.

Kikosi kilikuwa hivi; Yakoub Suleiman, Antony Mligo, Joshua Mutale, Alassane Kante, Shomari Kapombe, Morice Abraham, Rushine De Reuck, Naby Camara, Wilson Nangu, Elie Mpanzu na Neo Maema.

Waliotokea benchi ni Ahoua, Ladack Chasambi, Sowah na Mukwala waliochukua nafasi za Mutale, Kante, Morice na Camara.

Novemba 30 ilikuwa mechi ya mwisho Pantev akiwa Simba, hii ilikuwa ya pili ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika. Kichapo cha 2-0 ugenini kilihitimisha safari ya Pantev ndani ya Simba. Kabla ya mechi hiyo, Pantev alisema atakuwa na mabadiliko ya kimbinu kwa sababu anakutana na timu tofauti na ilivyokuwa ile ya kwanza. Hapa akaamua kuanza na mshambuliaji halisi.

Mechi hii kulikuwa na mabadiliko ya wachezaji wawili pekee, Ahoua na Mwalimu walianza badala ya Kante na Morice.

Alianza na kikosi hiki; Yakoub Suleiman, Antony Mligo, Joshua Mutale, Jean Charles Ahoua, Shomari Kapombe, Rushine De Reuck, Naby Camara, Wilson Nangu, Elie Mpanzu, Neo Maema na Seleman Mwalimu.

Walioingia ni Chamou, Kante, Sowah, Mukwala na Morice wakichukua nafasi za Mutale, Ahoua, Rushine, Maema na Mwalimu.

Muda mchache baada ya kusitishiwa mkataba kwa makubaliano ya pande mbili, Pantev aliteta na Mwanaspoti akisema hana kinyongo juu ya uamuzi huo.

“Kuhusu kuondoka kwangu Simba, hakukuwa na utata wowote. Kila kitu kilijadiliwa kwa uwazi na weledi tukakubaliana kwa pamoja kuwa, huu ulikuwa wakati sahihi kwa pande zote mbili. Sina kinyongo chochote dhidi ya klabu, ninathamini sana namna mchakato mzima ulivyoendeshwa,” alisema Pantev na kuongeza: “Nilikaa siku 61 Msimbazi na nakumbuka kila siku kama somo jipya.

“Sitasahau mazingira ndani ya klabu, mapokezi kutoka kwa mashabiki, pamoja na roho ya kupambana iliyo ndani ya timu. Hata baada ya kupoteza mechi mbili za hatua ya makundi dhidi ya Petro na Stade Malien, bado niliuona uwezo na ubora mkubwa ndani ya kikosi.

“Ninaondoka nikiwa na heshima kubwa kwa uongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki. Ninaitakia Simba kila la heri katika safari yake ya mbele.”

Hata hivyo, Pantev anaamini kwamba, kama angeendelea kupewa muda zaidi kuna vitu angevibadili ndani ya timu hiyo na kupata matokeo mazuri.

“Pamoja na hayo yaliyotokea, ninaamini ningepewa muda zaidi ningebadili mwelekeo wa timu.

“Ukiangalia usajili wa dirisha dogo ulikuwa unakuja, nilipanga kuongeza wachezaji watatu ambao tungekuwa katika hatua nyingine.”