Arusha. Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu Sebastian Kolowa (Sekomu), wameamriwa kuulipa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), malimbikizo ya michango ya wafanyakazi wake ya Sh678.4 milioni.
Fedha hizo ni malimbikizo ya michango ya wafanyakazi kwa kipindi cha kuanzia Septemba 2015 hadi Machi 2020.
Uamuzi huo umetolewa na Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Tanga, katika hukumu ya maombi ya madai namba 7/2020 yaliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa NSSF.
Hukumu hiyo imetolewa Desemba 3, 2025 na Jaji Katarina Mteule, aliyesikiliza shauri hilo na nakala ya uamuzi huo kupakiwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Rekodi za mahakama zinaonyesha Agosti 29, 2007 mdaiwa wa pili alisajiliwa rasmi kama mwajiri mchangiaji na alipewa cheti cha uanachama namba 721050, hivyo alikuwa na wajibu wa kutuma michango ya wafanyakazi kila mwezi.
Kumbukumbu za mahakama katika hukumu zinaonyesha kuanzia Septemba 2015 hadi Machi 2020 alishindwa kuwasilisha michango hiyo.
Kutokana na hilo, mdai alifanya ukaguzi na kutuma notisi ya madai na kwa nyakati tofauti mdaiwa wa pili alikiri deni hilo.
Katika maombi hayo, mdai aliomba mahakama iamuru alipwe Sh678.4 milioni ambazo ni michango ya wanachama na riba ya asilimia 15 kuanzia Septemba 2015 hadi tarehe ya hukumu, na riba ya jumla kwa kiwango kilichowekwa cha mahakama cha asilimia saba kuanzia tarehe ya hukumu hadi deni litakapoisha pamoja na gharama za kesi.
Imeelezwa wadaiwa walipatiwa hati za wito lakini walipuuza na kushindwa kujitetea mahakamani.
Baada ya kusikiliza hoja za upande mmoja, mahakama iliridhika kuwa mjibu maombi wa pili ameshindwa kutekeleza wajibu wake wa kisheria na hana utetezi kwenye rekodi, hivyo imeamuru wadai kulipa Sh678.4 milioni za michango ya wanachama ambayo haijarejeshwa pamoja na malimbikizo ya adhabu zinazopaswa kulipwa.
