Dar es Salaam. Mkuu wa Chuo cha Kimataifa cha Kampala Tanzania (KIUT), Profesa Peter Msolla ameonya matumizi kupita kiasi ya akili mnemba (AI) kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, akisema yanafifisha uwezo wao wa kufikiri.
Amesema kasi ya maendeleo ya uchumi hutegemea zaidi maarifa na ujuzi, hivyo ni muhimu wahitimu wa vyuo vikuu kutumia elimu waliyoipata kuchangia maendeleo ya nchi.
Aidha, amebainisha juhudi za Serikali kuboresha sekta ya elimu zimeongeza kasi ya mahitaji ya elimu ya juu na kuchochea uwekezaji katika chuo hicho.
Profesa Msolla ameyasema hayo leo Alhamisi Desemba 4, 2025 katika mahafali ya nane ya KIUT yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo zaidi ya wanafunzi 1,484 wametunukiwa ngazi mbalimbali za elimu.
“Tunaishi katika ulimwengu wa kidijitali tujihadhari na matumizi ya akili mnemba, siku hizi walimu wakitoa tu kazi mwanafunzi anakwenda anabonyeza anapata taarifa anayohitaji, hii linakwenda kufifisha ufikiri wanafunzi kwa hiyo kila kinachokuja kina hasara na faida zake.”
“Ni matumaini yangu kuwa ufaulu wenu ni ushahidi kuwa mmepata maarifa katika fani mlizosomea, jamii inataraji mna upeo wa hali ya juu katika kupambana na changamoto zinazokwamisha maendeleo, lakini uthibitisho utakuwa kwenye utendaji wenu huko mwendako,” amesema.
Akizungumzia maboresho ya chuo hicho, Profesa Msolla amesema tayari wameweka mipango ya kukamilisha hospitali ya chuo hicho kufikia mwishoni mwa mwaka 2026.
Amesema hospitali hiyo itatoa huduma kwa jamii na kuwa kituo cha mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi.
“Baraza la chuo limedhamiria kuboresha miundombinu ya kujifunzia kama maabara, viwanja vya michezo pamoja na hosteli,” amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Honoratha Mushi, amesema chuo kimeboresha miundombinu ya kufundishia, maabara, vifaa vya kisasa na ubora wa rasilimali watu.
Pia amesema KIUT imejipanga kuongeza uwezo wa kudahili ili kuunga mkono juhudi za Serikali ambazo zimekuwa kubwa katika sekta ya elimu.
Profesa Mushi amesifu juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, ambayo yameipa uhakika bodi ya chuo kuendelea na uwekezaji.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Profesa Yunus Mgaya, amesema kuongoza chuo kikuu binafsi kinachotoa elimu ya sayansi na teknolojia si jambo dogo, kwani kunahitaji rasilimali watu, fedha na uongozi madhubuti unaofuata sera, sheria na kanuni za elimu ya juu.
“Uongozi wa chuo unaendelea kuonyesha weledi, maoni na uadilifu. Baraza la chuo limefarijika na mafanikio haya na linaamini uongozi bora utaendelea kuleta matunda zaidi,” amesema.
Kati ya wahitimu 1,484 waliotunukiwa ngazi mbalimbali za elimu, 772 ni wanaume na 712 ni wanawake. Wenye vyeti vya stashahada ni 821, ambapo wanaume ni 381 na wanawake 440. Wenye shahada ya kwanza ni 641 na wenye shahada ya uzamili ni 22 pekee.
