Morogoro. Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limewakamata madereva watano wa magari ya kubeba wagonjwa (ambulance) waliokuwa wakitumia magari hayo kubeba abiria wasio na dharura, kinyume cha taratibu na sheria za usalama barabarani, hali inayotafsiriwa kuongeza hatari kwa watumiaji wa barabara.
Akizungumza na wanahabari leo Desemba 4, 2025, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema madereva hao walinaswa kupitia operesheni maalumu ya kuimarisha usalama barabarani kuelekea mwishoni mwa mwaka ili kupunguza ajali na makosa ya barabarani.
Amewataja waliokamatwa kuwa ni George Ming’ongo (29) mkazi wa Arusha, aliyekamatwa akiendesha gari aina ya Toyota Land Cruiser likiwa na abiria wanane; Paul Zacharia (37) wa Dar es Salaam aliyekuwa na abiria tisa katika gari jingine aina Toyota Land Cruiser; na Godliving Emmanuel Sawe (37) wa Dar es Salaam aliyekutwa na abiria 12 kwenye Toyota Hiace.
Mwingine ni John Masae (26) mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam, aliyekamatwa na abiria watano kwenye Toyota Land Cruiser.
Mkama amesema kitendo cha magari ya wagonjwa kubeba abiria wasio wa dharura ni ukiukaji wa sheria na huongeza hatari ya ajali.
Katika operesheni hiyo, Polisi pia imemkamata Omary Mussa Mbaga (34), mkazi wa Dar es Salaam, aliyekuwa akitafutwa kwa kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha vifo vya abiria watatu katika ajali iliyotokea Novemba 23, mwaka huu eneo la Iyovi kata ya Mikumi.
Amesema Mbaga alikuwa akiendesha basi aina ya Yutong la kampuni ya ABC na alitoroka baada ya ajali iliyotokea baada ya kupita magari mengine kwenye kona yenye alama ya tahadhari.
Jeshi hilo pia linamtafuta dereva mwingine, Athuman Mbuli, aliyetoroka baada ya kuhusika katika ajali ya kupinduka kwa gari aina ya Tata usiku wa Desemba 3, katika eneo la Mavimba wilayani Ulanga.
Katika ajali hiyo, abiria wawili wanafunzi wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari Nawenge, Christopher Mwambile (19) na Said Rajab (20) walijeruhiwa na kuvunjika mikono ya kushoto.
Wakati huo huo jeshi la polisi linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za mauaji katika matukio mawili tofauti ndani ya Manispaa ya Morogoro na wilayani Mvomero.
Mtu wa kwanza ni Joseph Hassan (35) mkazi wa mtaa wa Nguvukazi, Kihonda akiwa anatuhumiwa kumuua, Patrick Nachonda (50) kufuatia ugomvi uliotokea wakati wakinywa pombe.
Tukio la pili linamhusisha Faustin Christina (39) mkazi wa Maguruwe wilayani Mvomero, anayedaiwa kumuua Justine Luanda (38) katika tukio lililotokea Novemba 30, 2025, kitongoji cha Bonde, kata ya Bunduki.
Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mtuhumiwa alimshambulia marehemu kwa kitu butu kichwani baada ya ugomvi uliochochewa na ulevi.
Kamanda Mkama amesema uchunguzi dhidi ya matukio hayo unaendelea na hatua za kisheria zitachukuliwa.