DAR City (DSM) na Fox Divas (Mara), zimeonyesha ubabe katika Ligi ya Kikaku ya Taifa (NBL), inayofanyika kwenye Uwanja wa Chinangali, Dodoma na kudhihirisha uwekezaji unalipa.
Timu hizo ambazo zinatajwa kuwekeza katika kusajili wachezaji bora, Dar City iliyoanza uwekezaji huo mwaka 2022, ikishiriki ligi ya kikapu ya daraja la kwanza mkoa wa Dar es Salaam, na mwaka huo ikapanda daraja, chini ya kocha Mohamed Mbwana ilizifunga Dom Spurs kwa pointi 53-45, BBC kutoka Arusha kwa pointi 104- 47, Planet ya Mwanza 106-45, Kisasa Heroes (Dodoma) 74-62 na Manyara 123-45.
Kwa upande wa Fox Divas ambaye pia ni bingwa mtetezi, inaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wachezaji kutoka nje ya mkoa wa Mara, pamoja na wa kimataifa.
Kuwa na wachezaji hao, imetokana na kutofanyika Ligi ya mkoa huo tangu 2023, inaonyesha endapo ligi ingefanyika, ingeifanya timu hiyo iwe na wachezaji wake .
Baadhi ya wachezaji waliowasajili katika Ligi ya NBL ni pamoja na Anamary Cyprian, Witness Mapunda (Jeshi Stars) na Dina Mussa (Ukonga Queens).
Katika michezo ya Ligi hiyo iliyocheza iliishinda Orkeeswa (Arusha) kwa pointi 82-31, JKT Stars (DSM) pointi 81-76, Vijana Queens (DSM) pointi 69-50 na Bright Queens (Dodoma) kwa pointi 116-22.
Timu za JKT (DSM), Pamoja BBC (Arusha) , Planet (Mwanza), Orkeeswa (Arusha), na upande wanawake Bright Queens, JKT Stars zimeshirikisha wachezaji wake wazawa.
Wakati huo huo, kocha wa kikapu kutoka Temeke Joseph John ameiomba kamati ya ufundi na mashindano ya Ligi ya kikapu ya taifa (NBL), ifuate sheria na kanuni za usajili ya wachezaji wa kigeni.
“Kama wachezaji wa kigeni wanatakiwa 6 waruhusiwe na kama tunataka kuendeleza mchezo wa kikapu nchini, tunatakiwa tuwape nafasi na wachezaji wazawa waliocheza ligi,” alisema John.
