Dar es Salaam. Zaidi ya Sh5 bilioni zumelipwa kama fidia ya uharibifu wa mali kwa wateja zaidi ya 1,000 wa Kampuni ya Bima ya CRDB Insurance Company (CIC).
Hayo yalibainishwa katika mkutano uliowakutanisha Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela na menejimenti pamoja na wafanyakazi wa CIC jijini humo.
Akizungumza katika mkutano huo leo, Nsekela ameipongeza CIC kwa ufanisi wake wa umakini na jitihada za kuhakikisha wateja hawaumii kiuchumi pindi wanapopata majanga.
“Mwenendo huo naamini utaongeza imani ya Watanzania kutumia huduma za bima ambazo ni muhimu zaidi pale mhusika anapopata janga hasa uharibifu wa mali zake. Bila kuwa na bima, wengi huangukia kwenye umaskini lakini wale wenye bima huwa hawaumii sana,” amesema Nsekela.
Ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanalindwa na bima, Nsekela ameitaka CIC kutoa elimu kwa umma na kuzitangaza huduma walizonazo kwa kuwa, kufanya hivyo kutaongeza uelewa wa wananchi, hivyo kuwashawishi kuzitumia huduma hizo.
“Kila mtu huhitaji taarifa sahihi kabla hajatumia fedha zake. Nawasihi mjitahidi kutoa elimu kwa wananchi wengi kadri iwezekanavyo ili kuongeza idadi ya wateja,” amesema.
“Watu wengi wanapoteza mali zao na kujikuta wakianza upya kutokana na kutokuwa na elimu ya bima. Nendeni mpaka vijijini waliko wananchi wengi zaidi na mfikishe elimu ya huduma zinazotolewa na CIC pamoja na faida zake,” amesisitiza Nsekela.
Nsekela anayasema hayo wakati kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi ya mwaka 2024 iliyotolewa na Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, mauzo ya bima za kawaida yaliongezeka kwa asilimia 12.7 hadi Sh1.099 trilioni kutoka Sh974 bilioni mwaka 2023.
Katika mwaka huo, bima ya vyombo vya moto iliingiza Sh384.8 bilioni ikifuatiwa na bima ya moto (Sh189.9 bilioni) na afya (Sh162 bilioni).
Bima za maisha pia, ziliongezeka kwa asilimia 9.8, hadi kufikia Sh290.5 bilioni kutoka Sh264.5 bilioni.
Watoa huduma wa bima waliongezeka hadi kufikia 2,208 kutoka 1,549 mwaka 2023 (ongezeko la asilimia 42.5) kutokana na kurahisishwa kwa usajili, matumizi ya mifumo ya kidijitali na huduma mpya.
Ingawa kampuni za bima zilibaki 35, mauzo ya jumla yalipanda hadi Sh1.418 trilioni.
Mkurugenzi Mtendaji wa CIC, Wilson Mnzava amesema licha ya mwaka huu kuongeza idadi ya wateja wanaowahudumia, baadhi yao walipata changamoto zilizosababisha uharibifu wa mali zao.
Hiyo ililazimu kampuni hiyo kuwafidia ili kuwaondoa kwenye mkwamo ambao ungejitokeza.
“Mpaka mwishoni mwa Oktoba mwaka huu, tumesajili jumla ya wateja 43,977 waliotupa imani ya kuzilinda mali zao na kati yao wateja 833 walipata majanga ya uharibifu wa mali walizonazo,” amesema.
Ili kuhakikisha wanaendelea kuwa salama, amesema walilipa fidia ya Sh5.3 bilioni kwa mwaka 2026 na wamejipanga kuendelea kuwahudumia wananchi wengi zaidi ili kushiriki kuulinda uchumi wa nchi.
Hiyo imechangia kuendelea kuimarika na kampuni hiyo imetengeneza faida baada ya kodi ya Sh2.7 bilioni.
“Mafanikio haya tumeyapata kutokana na ushirikiano uliopo kati ya menejimenti na wafanyakazi. Wakati wote tumekuwa tukishirikiana kujenga umoja unaoleta ubunifu na kujitoa katika kuwahudumia wateja wetu.
“Tunafurahi kuona tunakidhi mahitaji na matarajio ya wateja wetu na tunawakaribisha Watanzania wengi zaidi kuja kuzitumia huduma zetu,” amesema Mnzava.
