USIKU wa jana Simba ilikuwa uwanjani ikiumana na Mbeya City katika mechi ya Ligi Kuu Bara, lakini gumzo mtaani na hata mtandaoni ni ishu ya Seleman Matola, kocha msaidizi anayekaimu ukocha mkuu kwa sasa katika timu hiyo.
Ndiyo, Matola ndiye aliyeiongoza timu katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo baada ya Dimitar Pantev kusitishiwa mkataba mapema wiki hii, ikiwa ni siku chache tangu Simba ipoteze mechi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba iliyopo Kundi D, ilianza na kipigo cha 1-0 mbele ya Petro Atletico ya Angola kisha 2-1 kwa Stade Malien na kuufanya uongozi kumtema Pantev aliyeajiriwa Oktoba 3 mwaka huu kama Meneja Mkuu, japo ndiye aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo.
Uongozi wa Simba ulitangaza kuachana na Pantev na wasaidizi aliokuja nao na unatafuta kocha mkuu mpya, lakini Matola akiendelea kusalia na kuzua gumzo, baadhi wakihoji kwa nini hapewi timu moja kwa moja na wengine kuhoji sababu za kubakizwa kila wenzie wanapotimuliwa.
Nyota na nahodha huyo na zamani wa Simba na Taifa Stars, alitua Msimbazi kama kocha msaidizi, Desemba, 2019 akitokea Polisi Tanzania na tangu hapo jamaa amefanya kazi na makocha tisa wa kigeni na mmoja mzawa.
Kila kocha mkuu anayeajiriwa Simba, Matola huwa msaidizi na kocha mkuu husika akiondoka klabuni kwa kufutwa kazi au kwa dili zake binafsi, kocha huyo mwenye Leseni A ya CAF hukaimishwa timu, lakini hajawahi kupewa moja kwa moja awe kocha mkuu.
Kuna wanaoamini ni zamu ya Matola kupewa jumla timu kwani tayari aliyejiunga akiwa na kigezo cha kuwa msaidizi hadi sasa akikidhi kigezo cha kusimama kama kocha mkuu kutokana na kupata nafasi ya kusoma akiwa na klabu hiyo aliyoitumikia awali kama mchezaji na anaijua ligi ya Tanzania.
Hapa chini ni makocha waliopita na kufanya kazi na Matola kisha kumuacha klabuni, huku ikielezwa ni kati ya wanaoaminika na uongozi wa ufanisi wa kazi, nidhamu kubwa aliyonayo na heshima aliyojiwekea enzi akiitumikia timu hiyo mbali na vigezo alivyonavyo.
Dimitar Pantev aliyetambulishwa Oktoba 3 kama Meneja Mkuu mwenye taaluma ya ukocha, ameiongoza timu hiyo katika mechi tano za mashindano ikiwamo moja ya Ligi Kuu na nne za Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya juzi kusitishiwa mkataba.
Kutoka Oktoba 3, 2025 hadi Desemba 2, 2025 ni siku 61 zilizohitimisha maisha ya Mbulgaria huyo ndani ya Simba baada ya uongozi kusitisha mkataba kwa makubaliano ya pande mbili na Matola amekaimishwa na kuingoza timu kwa sasa ikielezwa anatafutiwa kocha mpya.
Septemba 22, 2025 mkataba wa Simba na Fadlu Davids ulifikia tamati baada ya kocha huyo raia wa Afrika Kusini kujiunga na Raja Casablanca ya Morocco aliyokuwa akiinoa awali kabla ya kuja Tanzania.
Kocha huyo ameondoka akiwa ameitumikia kwa siku 444 tu na kurejea Raja ambako siku za nyuma alikuwa kocha msaidizi.
Kuondoka kwa Fadlu na wasaidizi wanne kulitokea siku sita tu baada ya mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga ‘Dabi ya Kariakoo’ uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Septemba 16 na timu kubaki mkononi mwa Matola kabla ya kuletwa kwa Pantev.
Abdelhak Benchikha raia wa Algeria alijiunga na kikosi hicho Novemba 24, 2024 akitoka kuipa USM Alger ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuibwaga Yanga kwa faida ya mabao mengi ya ugenini baada ya sare ya 2-2 na kubeba pia CAF Super Cup kwa kuifunga Al Ahly ya Misri.
Simba ilisitisha mkataba na kocha huyo kwa kile kinachofahamu ni kutokana na matatizo ya kifamilia ya kuuguliwa huko Algeria, akiwa amedumu kwa siku 156 tangu alipotambulishwa akichukua nafasi ya Robero Oliveira ‘Robertinho’ na timu kuachwa chini ya Selemani Matola.
Tangu alipokuwa na Simba, Benchikha aliiongoza timu hiyo katika mechi 21 katika mashindano mbalimbali ikiwemo ya Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ligi ya Muungano iliyorejea mwaka huu. Katika Ligi Kuu aliiongoza mechi 11, timu ikishinda sita, kutoka sare tatu na kupoteza mechi mbili ikifunga mabao 18 na kufungwa manane.
Alitokea Vipers ya Uganda na kipigo cha mabao 5-1 cha Novemba 5, 2023 kutoka kwa Yanga kilikuwa ni cha kwanza kwa Roberto Oliveira ‘Robertinho’ tangu alipojiunga na timu hiyo Januari 3, 2023 na kudumu kwa siku 310 tu hadi Novemba 9 mwaka huo, lakini ikawa tiketi ya kuondoka na kumuacha Matola.
Juma Mgunda alikabidhiwa kijiti cha kuinoa Simba kama kocha wa mpito, Septemba 7, 2022 siku chache kabla ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo Mserbia Zoran Maki aliyedumu kwa siku 70 ikiwa sawa na mwezi mmoja na siku 10 tu.
Kibarua cha kwanza kwa Mgunda kilikuwa kuisimamia Simba katika mechi ya kwanza ya raundi ya awali za Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya Nyassa Big Bullets Malawi na kuibuka na ushindi wa 2-0 siku tatu tu baada ya kupewa timu, yakifungwa na Moses Phiri na John Bocco.
Katika mechi 16 za Ligi Kuu ambazo Mgunda aliiongoza Simba, alishinda 11, sare nne na alifungwa mchezo mmoja tu dhidi ya Azam FC, jumla ya pointi alizokusanya ni 34, huku tisa zikiwa za Zoran Maki na moja ya Seleman Matola, dhidi ya KMC zikitoka kwa sare ya mabao 2-2, hivyo timu hiyo ina jumla ya pointi 44.
Nje na mechi za Ligi Kuu Bara za Ligi ya Mabingwa Afrika alizozisimamia ameshinda zote na moja ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
Zoran Maki aliondolewa huku akikimbizana na rekodi ya aliyewahi kuwa kocha wa Yanga, Zlatko Krmpotic anayeshikiria rekodi ya kudumu kwa muda mchache kwenye timu.
Septemba 6. 2022 Simba ilitangaza kuachana na Zoran Maki alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja baada ya makubaliano ya pande zote mbili akiwa na timu kwa siku 67 na kumuacha Matola akijijengea ufalme ndani ya timu hiyo kutokana na kuiongoza timu kwa muda mrefu akiwa kocha msaidizi.
Zoran alitambulishwa June 28 kuchukua nafasi ya Pablo Franco na kuondoka Septemba 6 akiiongoza timu katika mechi mbili za Ligi Kuu alizoshinda dhidi ya Kagera Sugar (2-0) na Geita Gold (3-0).
Simba ilithibitisha kuvunja mkataba na kocha Pablo Franco Martin baada ya kutoa taarifa hiyo kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo mtandao wa Instragram huku pia wakimtakia kila la heri kocha huyo kwa kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa kombe la Mapinduzi na kufika robo fainali ya kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Kuondoka kwa Pablo kulikuja siku chache baada ya timu hiyo kuondoshwa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kwa kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mkoani Mwanza na timu kuachiwa Matola aliyekuwa msaidizi wake. Pablo alitua nchini kuchukua nafasi ya Mfaransa Didier Gomes Da Rosa aliyetimuliwa Oktoba 26, 2022.
Oktoba 26, 2021 SImba iliachana na Kocha Didier Gomes Da Rosa baada ya makubaliano ya pande mbili, siku chache baada ya timu hiyo kuondoshwa Ligi ya Mabingwa Afrika na Jwaneng Galaxy ya Botswana ilipokubali kichapo cha mabao 3-1, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Gomes alitua nchini akichukua nafasi ya Mbeligiji Sven Vandenbroeck ambapo alikiongoza kikosi cha Simba kwenye mechi 33 huku akishinda mechi 25, sare nne na kupoteza nne.
Kutokana na hatua hiyo, aliyekuwa Kocha msaidizi wa timu hiyo, Thierry Hitimana, ndiye aliyechukua mikoba ya Gomes akisaidiwa na Selemani Matola.
Huyu ndiye aliyekuwa kocha wa kwanza wa kigeni kufanya kazi na Matola mara baada ya kocha huyo mzawa kujiunga na Simba akitokea Polisi Tanzania.
Sven Vanderbroeck aliachana na Simba siku chache baada ya kushinda 4-0 kwenye Uwanja wa Mkapa dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe katika Ligi ya Mabingwa na kusonga hatua ya makundi na timu kuwa chini ya Matola kwa muda.
Aliondoka Simba ikiwa nafasi ya pili kwenye ligi baada ya michezo 15 na pointi 35 ikifungwa mbili na sare mbili ikishinda 11 na kutimkia FAR Rabat ya Morocco na Januari 24 Simba ikamtangaza Didier Gomes kama kocha mkuu akitokea El Merreikh ya Sudan
Kipa wa zamani wa Simba, Steven Nemes amesema Matola ana vigezo vyote vya kuwa kocha mkuu amepata nafasi ya kusoma akiwa na timu hiyo, hivyo ni muda sahihi kwa viongozi kumuamini kwa kumuachia timu.
Amesema wanaweza kumpangia hata mechi ili aweze kuonyesha alichonacho kutokana na kuwa na vigezo sambamba na uzoefu alioupata chini ya makocha aliofanya nao kazi na sasa ni muda sahihi kwake kujaribiwa.
“Wampe thamani wasiangalie uzawa anaweza akaitoa timu ilipo na kuifikisha mbali lakini kama wanavyofanya kwa makocha wa kigeni akiharibu pia ataondolewa kila kocha ana bahati yake,” amesema Nemes aliyetamba pia Yanga, Majimaji, Mtibwa Sugar na Taifa Stars aliyeongeza.
‘’Matola amekaa na makocha wengi wa kigeni ambao wamekuja na kuondoka, hivyo amepata uzoefu pia amekuwa akiachiwa timu anaifundisha kwa kusimamia mechi mbili tatu ni sehemu ya kipimo kuwa anauwezo wa kuisimamia na kuwa na mipango sahihi.”
Mshambuliaji wa zamani Simba, Zamoyoni Mogella amesema anashangazwa na uongozi wa timu hiyo kutumia ghalama kubwa kuleta makocha wa kigeni ambapo wakati mwingine wanakosa vigezo kwa kukosa imani na kocha mwenye uzoefu wa kutosha tangu amejiunga na timu hiyo.
Amesema Matola amepata uzoefu wa kutosha na anashangaa ni kwa nini uongozi unashindwa kumuamini huku akitolea mfano ya Juma Mgunda, aliyewahi kupita katika timu hiyo kuaminiwa tofauti na mkongwe aliyehudumu kwa muda mrefu.
“Simba kwa miaka ya karibuni imeingia hasara kubwa ya kuleta makocha ambao wanatumikia kwa muda mchache baadae wanawavunjia mikataba hasara hiyo ni ya kujitakia sasa ni wakati wa kumuamini Matola ili kupunguza gharama,” amesema Mogella aliyewahi kuitumikia Yanga na Stars.
‘’Matola ana uzoefu wa kutosha wamuamini kwa kumpa muda ikishindikana watakuwa wamejivua lakini kwa wanachokifanya sasa ni kuingia hasara zisizo na maana kwani tayari wana kocha ambaye tayari amepata uzoefu wa kutosha chini ya makocha 10 wa kigeni aliofanya nao kazi.”
Kwa upande wa Matola aliwahi kunukuliwa akisema kinachombeba ni ufanisi kazini, nidhamu na kujituma na kusikiliza uongozi unataka nini na pia rekodi akibaki na timu na kuwajua wachezaji.
