UONGOZI wa Mashujaa FC umemalizana na kiungo mshambuliaji wa Bigman FC, George Makang’a atakayeanza kuitumikia timu hiyo mara baada ya dirisha dogo kufungwa.
Makang’a ataingia katika mfumo wa Mashujaa rasmi na kutambulika kama mchezaji wa yimu hiyo baada ya dirisha dogo la usajiri ambalo linafunguliwa mwanzoni Januari mwakani.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya timu hiyo kimeliambia Mwanaspoti kuwa, ni kweli wamemalizana na mchezaji huyo tangu dirisha kubwa, lakini walichelewa kumuingiza katika mfumo na ndipo walipompeleka Bigman kwa mkopo wa miezi sita.
“Makang’a ni mchezaji wa Mashujaa mara baada ya dirisha dogo kufunguliwa atarudishwa atakuwa sehemu ya kikosi kinachopambania nafasi tano za juu msimu huu ukiangalia timu yetu imekosa kiungo mwenye uwezo wa kutengeneza nafasi na kufunga nafikiri akijiunga na timu yetu kuna kitu kitabadilika eneo la ushambuliaji,” amesema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Timu yetu ina mapungufu mengi eneo la ushambuliaji nafasi zinatengenezwa lakini hazitumiki hivyo mbali na Makang’a kutakuwa na usajili mwingine kwenye safu ya ushambuliaji na ulinzi.”
Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta Makang’a ili aweze kuzungumzia suala hilo amesema ni kweli ataitumikia Mashujaa kuanzia Januari baada ya kumalizana na uongozi wa timu hiyo.
“Ni kweli na sasa nipo naendelea na mazoezi binafsi nimeamua kuachana na Big Man nahofia kupata majeraha kwani mimi tayari ni mchezaji wa Mashujaa.”
Kiungo huyo amepita Lipili, Namungo, KMC na Mtibwa Sugar ambayo amemalizana nayo baada ya kupanda daraja.
