Dar/Mikoani. Uapisho wa madiwani katika maeneo mbalimbali nchini umefungua ukurasa mpya wa majukumu, matarajio na mitihani.
Pamoja na kupewa dhamana ya uwakilishi kwa miaka mitano, wajibu mkubwa umewekwa mezani: kusikiliza wananchi, kutatua migogoro, kusimamia miradi, kulinda amani na kuhakikisha halmashauri zinasonga mbele.
Katika kauli zilizotolewa na viongozi wa wilaya na mikoa, ujumbe unaojirudia ni mmoja: “Madiwani ndio kiungo cha kwanza kati ya Serikali na wananchi, hivyo hawawezi kukwepa mzigo huu.”
Wachambuzi wa masuala ya siasa kwa upande wao wanasisitiza kuwa, ingawa diwani hana fedha za utekelezaji, ana rasilimali muhimu kuliko zote ambayo ni nguvu ya ushawishi.
Kwa nyakati tofauti kuanzia Desemba 3, 2025 madiwani wamekuwa wakiapishwa baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Katibu Tawala wa Ilemela, Anna Mbao amewataka madiwani kutimiza wajibu wao kwa uadilifu na kuhakikisha wanawatumikia wananchi waliowachagua kwa kuwasilisha changamoto zao ili zifanyiwe kazi.
“Tunajua tumechagua viongozi bora ambao mtatendea haki nafasi zenu, kwani ninyi ni kiunganisha na kiwakilishi cha wananchi katika Serikali na halmashauri. Tunategemea mtawakilisha matamanio ya wananchi na vipaumbele vyao,” amesema.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi, Reuben Chongolo, amewarai madiwani kusikiliza zaidi wananchi kuliko kuwaamulia mambo bila kuwashirikisha. Amesema viongozi hao wanapaswa kubadilisha namna ya utendaji kazi wao kwa kuwasikiliza na kujadiliana na wananchi ili kujua mahitaji yao ya msingi.
“Sote tunafahamu tulipita katika mtikisiko kidogo kwa wale ambao tupo karibu na mji mtakuwa mnaelewa. “Twendeni kwa wananchi tukawasikilize na kujua mahitaji yao, kwa kufanya hivyo tutajua kitu gani wanahitaji kwa wakati huo,” amesema.
Amesema kila kiongozi ana wajibu wa kuhakikisha huduma bora zinatolewa ambazo zinaonyesha matokeo chanya na tija kwa wananchi, ikiwamo kusimamia fedha, kupanga mipango na utekelezaji wa mifumo mbalimbali kwenye miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Chongolo amewasisitiza madiwani kuhakikisha miradi ambayo haikukamilika kipindi kilichopita inakamilika kabla ya kuanzisha mipya ili ufanisi uonekane.
Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa amewataka kuweka masilahi ya wananchi mbele katika uamuzi na majukumu yao ya kila siku, akisisitiza dhamana waliyopewa ni ya kuwatumikia wananchi, si vinginevyo.
Amesema jukumu kuu la madiwani ni kusimamia na kuishauri ipasavyo menejimenti ya halmashauri, hivyo hawapaswi kusita kutoa ushauri, kufuatilia na kudai uwajibikaji pale inapohitajika.
“Mpo hapa kwa ajili ya wananchi. Kila mtakachokifanya, kiwe kwa masilahi ya wananchi waliowapa dhamana. Msisite pale mnapotakiwa kusimamia na kuishauri menejimenti ya halmashauri,” amesema Nzowa.
Vilevile, amesisitiza usimamizi madhubuti wa mapato ya halmashauri, akisema iwe ajenda ya kudumu katika vikao vyao, kwa kuwa mapato ni moyo wa halmashauri na nguzo kuu ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, amesema madiwani wana wajibu wa kufuatilia na kuisimamia ili ikamilike kwa wakati, kwa viwango na bila ubabaishaji.
Mbali ya hayo, amesema wanapaswa kwa kushirikiana na menejimenti kusimamia nidhamu na uwajibikaji wa watumishi, ili wasiowajibika wachukuliwe hatua.
Amewakumbusha kuhakikisha vikao vya kisheria kuanzia ngazi ya kata, vijiji na vitongoji vinafanyika kwa wakati na kutoa nafasi kwa wananchi kusikilizwa na kupata ufumbuzi wa kero zao.
Ajenda ya ulinzi na usalama amesema ni ya kudumu, akiwataka madiwani kutoa elimu kwa wananchi kuhusu thamani ya amani na kuchukua hatua mapema pale panapoonekana viashiria vya uvunjifu wa amani.
Nzowa amewahimiza kujisomea majarida, kanuni na sheria ili kuongeza uelewa na uwezo wa kuchangia hoja zenye tija zitakazosaidia kusogeza mbele maendeleo ya halmashauri na mkoa kwa ujumla.
Mbunge wa Bukoba Mjini, Jonhston Mtasingwa, ambaye kwa wadhifa wake anaingia kwenye baraza la madiwani, amewataka kuhakikisha wanakuwa kichocheo cha kutatua migogoro ndani ya jamii na kuongeza chachu ya mafanikio ya wananchi kwa kusimamia miradi ya maendeleo.
“Naomba madiwani wenzangu sisi tuliobahatika kuingia kwenye baraza hili tuhakikishe tunafanya kazi ya wananchi kwa kuwasikiliza waliyotuagiza. Naomba tuendelee kuhubiri amani kwa vijana wetu ndipo tutafanikiwa kuleta maendeleo,” amesema.
Katika hilo, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva, amehimiza usimamizi wa miradi ya halmshauri na mapato, akiwataka madiwani kuepuka migogoro isiyo na tija.
“Nawaomba madiwani twendeni tukafanye kazi kwa pamoja kwa kusimamia miradi ya maendeleo na mapato ya halmshauri, tusiwe watu wa migogoro mara kwa mara,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa, amehimiza matumizi mazuri ya nafasi zao kwa kuwatumikia wananchi, badala ya kusababisha migogoro kwenye maeneo yao.
“Kiongozi ni kioo kwa jamii anayoiongoza kwa sababu huwezi kuwa kiongozi halafu unakuwa chanzo cha migogoro katika eneo lako. Hivyo, niwaombe madiwani mnapaswa kuzingatia maadili ya viapo vyenu mnapokuwa kwenye maeneo yenu ya kazi,” amesema.
Matumizi ya fursa, uzalendo
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amewataka madiwani kutambua fursa zilizopo na kuzitumia ili halmashauri ipige hatua, akiwahimiza kuifahamu vema halmashauri yao ili kujua maeneo ya kuyafanyia kazi.
”Cha kwanza mjue ninyi ndiyo wenye halmashauri, mhakikishe mnaisimamia vyema, nendeni mkatimize wajibu wenu, wananchi wanahitaji matokeo kwa kipindi cha miaka mitano,” amesema.
Ni rai ya mbunge wa Mtama, Nape Nnauye kwa madiwani na watendaji kuwa wazalendo, hususani katika kutoa huduma bora kwa wananchi na kutumia lugha nzuri.
“Safari hii ninawaomba madiwani tuwe wakali kwa watendaji wetu, hasa katika kutoa huduma bora na lugha nzuri kwa wananchi,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Salmon, amesema ili baraza liwe na ufanisi, halipaswi kuwa tegemezi wala kushinikizwa, bali lizingatie wajibu wake wa msingi wa kuwatumikia wananchi.
Rai nyingine imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, ambaye amewataka madiwani kuwa tayari kuwatumikia wananchi kwa kutekeleza ahadi walizowaahidi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Chirukile amewataka kusimamia miradi ya Serikali na kubuni vyanzo vya mapato kwa ajili ya kuleta maendeleo.
“Wasikilizeni wananchi wana mambo mengi ya kuchangia kwenye maendeleo katika kata zenu msiwabague kwa sababu ya itikadi ya vyama, wapeni ushirikiano ili kuipaisha manispaa yetu na taifa kwa ujumla,” amesema.
Mchambuzi wa Sera za Umma na Utawala, Dk Rehema Mkwawa, amesema jukumu la msingi la diwani ni kuwa kiungo cha uhai kati ya Serikali na wananchi.
“Madiwani wanapaswa kuanza kwa kurejesha misingi ya uwakilishi. Wananchi wengi wamechoshwa na uwakilishi wa wakati wa uchaguzi pekee. Diwani anayenufaisha wananchi ni yule anayekaa nao mara kwa mara, kusikiliza matatizo yao na kuyaibua kwenye baraza la madiwani bila woga,” amesema.
Amebainisha changamoto nyingi za mitaa ni uhaba wa maji, miundombinu hafifu, usalama na usafi, ambazo mara nyingi hazihitaji miradi mikubwa bali usimamizi thabiti.
“Diwani anatakiwa kuwa mlinzi wa miradi ya maendeleo. Aisimamie, ahakikishe thamani ya fedha inaonekana na atoe taarifa kwa wananchi kwa uwazi. Pale fedha zinapopotea au mradi unaposuasua, sauti yake ndiyo inapaswa kuwa ya kwanza kusikika,” amesema.
Amesema madiwani wanapaswa kuwa mabalozi wa mapato ya ndani ya halmashauri akisisitiza: “Maendeleo hayawezi kutokea kama halmashauri hazikusanyi mapato ipasavyo. Madiwani lazima wasimamie mbinu za kuongeza mapato bila kuwaumiza wananchi.”
Ni mtazamo wa mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Hassan Mchome kuwa, wananchi kwa sasa wanahitaji madiwani wanaofikiri nje ya siasa za kawaida.
“Madiwani wengi wanakwama kwa sababu wanaingia kwenye migogoro ya kisiasa na kusahau majukumu ya msingi. Diwani wa karne hii anapaswa kuwa msuluhishi, si mshabiki,” amesema.
Kuhusu huduma za kijamii, Profesa Mchome ameeleza diwani anapaswa kuwa msimamizi wa ubora.
“Shule zimeelemewa, zahanati hazina vifaa, barabara za mtaa hazipitiki madiwani wana uwezo wa kuzisimamia kamati za huduma, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kutoa mapendekezo ya kinadharia na vitendo. Wanapaswa kutumia takwimu, si hisia,” amesema.
