Chalamila ataja mambo sita yanayolalamikiwa na wananchi

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila ametaja malalamiko sita ya wananchi yanayodaiwa kuongeza chuki baina yao na Serikali, likiwemo suala la utekaji.

Mambo mengine ni wananchi kutosikilizwa, ukosefu wa ajira kwa vijana, viongozi kuishi maisha ya starehe, matumizi mabaya ya rasilimali za Serikali na matumizi ya nguvu kupita kiasi.

Chalamila ametoa kauli hiyo leo, Desemba 4, 2025, katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), juu ya athari za vurugu za Oktoba 29, 2025.

“Hata sisi kwa Mkoa wa Dar es Salaam, tunalaani vitendo vya utekaji; lipo tukio moja limewahi kutokea la kijana mmoja anapakizwa kwenye gari… ukiangalia lile tukio, pamoja na mambo mengine, yalikuwa masuala ya mapenzi,” amesema.

Chalamila amesema uchunguzi wa matukio ya utekaji upo na kuna yanayofanyika haraka na mengine yanayochukua muda kulingana na mazingira ya tukio husika.

Kuhusu ajira kwa vijana, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo kutokana na ongezeko la wahitimu, lakini amegusia baadhi ya vijana wanamiliki simu za gharama, wakishindwa kujishughulisha na biashara ndogondogo za kuwaingizia kipato.

“Wananchi kutosikilizwa, si kweli kwamba hatuwasikilizi raia, nikikaa hapa naweza kupokea simu zaidi ya 50. Wengine wanatuma ujumbe ‘we mkuu wa mkoa nakuja kwako karibu mara tano kuomba, lakini ukienda kwenye misiba unatoa michango, maana yake unapenda sana watu waliokufa’,” amesema.

Katika hatua nyingine, Chalamila amesema Serikali haijibizani na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kauli hiyo ikiwa ni jibu la swali la mwandishi aliyehoji ni kwa nini Serikali imekuwa ikiyajibu matamko ya baraza hilo badala ya kuyafanyia kazi.

Swali hilo limekuja, baada ya Chalamila kutumia waraka wa TEC katika mazungumzo yake, akionekana kama analijibu baraza hilo kuhusu matukio ya Oktoba 29, huku akirejea pia Rais Samia alivyouzungumzia waraka huo.

“Waraka wa TEC ni wa ushauri na yapo mambo mengi ya ushauri, kwa la Katiba mpya siyo suala la Serikali bali ni la wananchi. Serikali haijibizani hata kidogo, maelezo ya Rais ni kwamba vyombo vya dini viendelee kutumika kuunganisha wananchi. Rais kurejea waraka wa TEC maana yake ameusoma,” amesema.

Kuhusu madai ya Padri Kitima kuhusu kukatika kwa umeme sambamba na tukio la kushambuliwa kwake, akihisi tukio hilo kama la kupangwa, Chalamila amesema, “Kwa kuwa Tanesco inatajwa kwenye masuala hayo, lazima kuangalia kama kuna vijana wao wanahusika na hayo, kama sivyo, Tanesco itaendelea na masuala ya kisheria kuhusu mambo hayo.”

Akizungumzia matukio ya utekaji, amesema Serikali ya mkoa inalaani matukio hayo. Akijibu swali la mwandishi kuhusu iwapo amewahi kufika nyumbani kwa mama yake aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, kumjulia hali baada ya kiongozi huyo kutekwa, amesema hajawahi.

Chalamila amesema kama kiongozi ni vigumu kutembelea kila mtu na hata hivyo alikiri kutokuwa na taarifa za Polepole kuwepo nchini, akidokeza taarifa zake alikuwa akizipata mtandaoni kama wengine.

“Sina Connection (muunganiko) na maisha ya Polepole. Polisi wapewe muda; kama walivyosema wanaendelea kufanyia kazi,” amesema Chalamila.

Akizungumzia suala la ajira, Chalamila amesema Serikali inaendelea kutengeneza mazingira ya ajira kwa vijana na ndiyo maana Rais Samia akaunda wizara inayohusika na vijana pamoja na kutoa mikopo ya asilimia 10.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema majukumu yao ni kuhakikisha amani inakuwepo nchini kwa kushirikiana na wananchi.

Naye Mhariri wa Kituo cha Habari Clouds, Joyce Shebe amesema katika vyombo vya habari zipo changamoto zinazoikumba sekta hiyo, ikiwemo mazingira bora ya kazi.

Amerejea vurugu za Oktoba 29, akisema mazingira kwa waandishi hayakuwa mazuri, akiomba Serikali iangalie sheria zinazoiumiza sekta hiyo ili mazingira ya kazi yawe bora.

Mapema akichokoza mada, Mwenyekiti mstaafu wa TEF, Absalom Kibanda ameshauri Polisi kuruhusu vyombo vya habari kuripoti matukio kama ya Oktoba 29 kwa uhalisi wake, akisema kama vinginekuwepo madhara yake yangepungua.