Meya Jiji la Mbeya akemea majungu, atao msimamo

Mbeya. Meya Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa amewataka madiwani  kujenga heshima kwa  viongozi wa chama na Serikali kwa kuhepuka majungu, mifarakano na  kuwa sehemu ya kuijenga halmashauri mpya.

Katika hatua nyingine ametangaza msamaha kwa wale walio mkosea kwa kufungua ukurasa mpya wa safari ya miaka mitano na kuwahakikisha kutoa ushirikiano.

Issa amesema hayo Desemba 5, 2025, mara baada ya kutangazwa kushika nafasi hiyo kwa awamu ya pili na kuwa miongoni mwa madiwani walio apishwa kwenye kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa City Peack jijini hapa.

Kikao hicho kilihusisha madiwani 45 kati ya 55 wa Jimbo la Mbeya mjini na Uyole  sambamba na kufanya uchaguzi wa Meya, Naibu Meya na kamati maalumu za kudumu.

“Baraza hili linapaswa kuwa la mfano tulinde heshima za viongozi na wabunge  kwa kutambua tuna majimbo mawili  watatushangaa wakiona tunafarakana badala ya kuwa wamoja katika kuleta chachu ya kuibua miradi mipya yenye mchango kwa  halmashauri,”amesema.

Katika hatua nyingine ametumia fursa hiyo  kutangaza  msamaha kwa wale walio mkosea na wanahisi  aliwakosea  kumsamehe huku akisisitiza hataki majungu yeye anamtegemea Mungu.

“Madiwani wenzangu ambao mmechaguliwa kwenye kamati msiwe chanzo cha kutugawa au kugawanyika kama ujapata leo, kesho utapata ni suala la muda cha msingi kushirikiana ili kuwa na baraza la madiwani la mfano,”amesema.

Issa amesema anafunga milango ya kupokea majungu na kuhitaji madiwani kujenga hoja za kuleta maendeleo katika Jimbo la Mbeya Mjini na Uyole.

“Ndugu zangu kwangu milango ya majungu naifunga sitataka kuona diwani mmoja ananiletea hadithi za diwani mwingine, lakini atakaye nisema asemi mimi namtegemea Mungu,”amesema.

Issa amesema ufike wakati madiwani kuheshimiana kwa kuondoa makundi na kutozitwisha mzigo kamati za Chama cha Mapinduzi (CCM), kuwa sehemu ya kukaa kusuruhisha kesi mara kwa mara.

Katibu Tawala Wilaya ya Mbeya, Mohamed Aziz ameonya madiwani kuondoa tofauti zao na kuwataka kwenda kwa wananchi kusikiliza na kutatua kero zao.

Amesema hatua ya kula kiapo ni kujidhihilisha mnakwenda kushirikiana na halmashauri katika kuleta maendeleo sambamba na kuhakikisha mnawafikia wananchi.

“Madiwani ondoeni tofauti zenu nendeni mkaunge mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, tumeona na kusikia hotuba yake siku akiongea na wazee ameonyesha wapi tumetoka na tuendako kwa maslai mapana ya nchi,”amesema.

Diwani Kata ya Nsalaga, Clement Mwandemba amesema ni wakati  wa kuwatumikia wananchi kwa kuwafikia kuona changamoto hususani kwa kundi la vijana.

“Tumefika hapa kwa kuaminiwa na wananchi jukumu letu kurejea tena kukaa chini kuzungumza kujua wapi panahitaji kuwekwa sawa,”amesema.