BAADA ya vigogo vya soka Simba na Yanga kumaliza kazi juzi kwa ushindi nyumbani dhidi ya Fountain Gate na Mbeya City mtawalia, uhondo wa Ligi Kuu Bara unaendelea leo Jumamosi kwa mechi mbili za kibabe ikiwamo ya Singida Black Stars dhidi ya TRA United.
Juzi Yanga iliikandika Fountain kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa KMC Complex, huku Simba ikishinda 3-0 mbele ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na kujiweka pazuri zikisubiri kesho Jumapili kushuka tena uwanjani dhidi ya Coastal Union na Azam FC.
Mechi ya Singida na TRA inatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni, ilihali mapema saa 8:00 mchana Pamba Jiji itakuwa wageni wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
Singida inakutana na TRA ikiwa imetoka kulazimishwa suluhu na Azam, wakati wapinzani wao wakitoka kupasuka 2-1 mbele ya Mtibwa Sugar, mechi zote zikipigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam.
Pambano hilo la jioni linatarajiwa kuwa gumu kutokana na rekodi ya mechi nne zilizopita baina ya timu hizo, kwani mbili ziliisha kwa Singida kutoka na ushindi zote ikiwa nyumbani, huku nyingine za ugenini zikimalizika kwa sare, ikiwa maana TRA (zamani Tabora United) haijaonja ushindi.
Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana katika Ligi Kuu msimu uliopita Singida ikiwa nyumbani ilishinda kwa mabao 3-0 kupitia Victorien Adebayor aliyefunga la kwanza na Jonathan Sowah aliyepo Simba kwa sasa kutupia mengine mawili na kuizima TRA United.
Licha ya rekodi iliyonayo Singida nyumbani dhidi ya TRA, bado inaweza kukutana na ugumu kwa vile wageni wao wametoka kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu ikiwa ugenini mbele ya Mtibwa iliyowanyoa 2-1 na JKT Tanzania iliyowachapa 1-0.
Ikiwa chini ya kocha mpya, Etienne Ndayiragije huenda TRA haitakubali tena kuendelea kugawa pointi tatu, japo itakuwa na kazi mbele ya vijana wa Miguel Gamondi anayewategemea nyota kama Khalid Aucho, Clatous Chama, Elvis Rupia, Marouf Tchakei na wengine kuendelea ubabe.
TRA itaendelea kuwategemea Adam Adam, Salum Chukwu, Fode Konate, Joseph Akandwanaho na Ramathan Chobwedo mwenye bao moja kuizima Singida ili ijitoe eneo la chini la msimamo, kwani kwa sasa ina pointi sita baada ya mechi sita ikiwa na wastani wa pointi moja kila mechi.
Singida iliyocheza mechi nne imekusanya pointi nane ikishika nafasi ya 10 ikitenganishwa na TRA kwa tofauti ya pointi mbili na kama itateleza leo itakuwa na maana wageni watawapiku kwa kufikisha pointi tisa na kuwaporomosha. Rekodi zinaonyesha mara ya mwisho kwa TRA kushinda ugenini ilikuwa Februari 11, mwaka huu dhidi ya Kagera Sugar iliyowachapa mabao 2-1 katika Ligi ya msimu uliopita ambao wenyeji wao hao walishuka daraja sambamba na Ken Gold kwenda Ligi ya Championship.
Ukiacha mechi hiyo ya jioni , mapema mchana kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya maafande wa Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wa Pamba Jiji katika mechi nyingine ngumu ya Ligi Kuu.
Hii ni mechi ya tatu kwa timu hizo katika Ligi Kuu, ambapo mbili zilizopita zilizoigwa mwaka jana Prisons ilishinda moja ya nyumbani na nyingine ya ugenini ikiisha kwa sare zote, jambo inalotoa picha kwana mechi ya leo huenda ikawa ngumu kwa timu zote.
Pamba iliyotoka kushinda mechi mfululizo za nyumbani inasaka ushindi ili kurejea kileleni kwani kwa sasa ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 15 nyuma ya JKT Tanzania yenye 17 na ikiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi wa chee katika mechi ya mwisho ya ugenini dhidi ya Dodoma Jiji iliyopigwa Oktoba 25.
Prisons iliyotoka kupoteza mechi mbili za ugenini, yenyewe itakuwa inasaka ushindi wa tatu katika ligi ya msimu huu, kwani katika mechi sita ilizocheza imepoteza nne, huku mbili ikishinda ikiwamo ya ugenini dhidi ya Mbeya City iliyowachaopa 2-1 na ile ya nyumbani dhidi ya KMC iliyoilaza 1-0.
Timu zote zinafundishwa na makocha wa kigeni kutoka Kenya, wenyeji wakiwa na Zedekiah Otieno huku Pamba wakiwa na Francis Baraza, hali ambayo inalifanya pambano kuwa gumu, licha ya kila moja msimu huu kuonekana kuwa tofauti tangu Ligi ilipoanza Septemba 17 mwaka huu.
Pamba inamtegemea kinara wao wa mabao Peter Lwasa aliyefunga matatu, Mathew Momanyi mwenye mawili, mbali na Ben Mwakibinge na Mohammed Camara, wakati Prisons nyota tegemeo ni Jeremiah Juma, Haruna Chanongo na Oscar Mwajanga wenye bao moja kila mmoja.
