Mume wangu anafanya kazi nzuri na anapata mshahara na marupurupu ya maana, ila kila nikimwambia tufanye maendeleo haonyeshi ushirikiano.
Ninashukuru nikimuomba pesa ananipa, ila kujipanga kwa ajili ya maisha ya baadaye ni ngumu hata kujenga kibanda cha kuishi hafikirii . Tunapanga nyumba za ambapo tungejiongeza kidogo tu tungejenga ya kwetu tena ya maana.
Nilipobaini kuwa hashawishiki kujenga nilijichanga pesa zangu na alizokuwa akinipa nimejenga nyumba ndogo lakini nzuri na ina kila kitu. Sitaki kuitumia kuishi nataka uwe uwekezaji kwa sababu sina biashara ya kueleweka inayoniingizia kipato.
Ila changamoto niliyonayo ni kwa namna gani nitamueleza mume wangu kuhusu nyumba na nifanyeje akisema tukaishi humo?
Kila siku nasema hakuna jambo linalomalizika au kupata jibu kwa kulikimbia, mazungumzo ya busara ndiyo jibu la kila kitu.
Katika hili inategemea na unavyomjua mumeo, kama ni mtu wa jazba jipange kuzitulia mara tu utakapomwambia hili suala. Ila kama mwelewa kazi rahisi mno.
Ila kwa namna yoyote iwayo, lazima mazungumzo kuhusu hili suala yafanyike. Hivyo muandae kuwa unataka kuzungumza naye akiwa na nafasi. Wengi ukiwaambia hivi unaweza kuisubiri hiyo nafasi hadi mwakani, hivyo mwambie hivyo huku unajipanga kuzungumza naye pindi ukimuona ametulia na ana amani kabla hajakuambia amepata hiyo nafasi.
Wakati wa kuzungumza, ni muhimu kuwa mtulivu, thabiti na mwenye busara. Mweleze kuwa umejenga nyumba hii kwa nia njema na si kumficha au kuamua pekee, bali ni hatua ya busara ya kifedha na kumuonyesha ni kwa namna gani kila senti aliyokupa uliiwekeza kwa kuchanganya na za kwako.
Hakikisha unapozungumza unamjumuisha kwenye ujenzi wa hiyo nyumba aliokuwa haujui, ila kulikuwa na mchango wake kwa namna fulani. Hii itamfanya akusikilize na ajione ni sehemu ya huo ujenzi.
Hii haimaanishi kuwa nyumba itakuwa yake, kwani vibali vyote vitabaki kuwa vyako ila atatambua kuwa alikuwa na mchango.
Muhimu pia kuweka sawa taarifa zako za kifedha ili isije kuonekana hiyo nyumba labda umejengewa, yaani kusiwe na maswali kuhusu fedha za kujengea.
Pia bila kuchelewa mweleze unachofikiria kwenye hiyo nyumba kama ulivyosema unataka kiwe kitega uchumi. Hapa kwa mwanaume mwelewa atakuona unafikiria mbali na kukupongeza badala ya kung’ang’ania mkaishi humo.
Ukimueleza kinaga ubaga kuwa umefanya hivyo baada ya kuona huna kitega uchumi wala biashara ya kueleweka inayokuingizia kipato, hivyo kuna wakati unakosa ujasiri.
Pia tumia fursa hiyo kumueleza kuwa kujenga si mamilioni bali ni malengo. Hii inaweza kumshawishi kujenga nyumba yenu na kuondokana na kupanga.
Si hivyo tu bali pia inamfanya akuamini zaidi na pengine akakupa mradi wa kusimamia ujenzi wa nyumba za kupangisha kwani umesema fedha anayo.
Hii pia inaweza kuwa msukumo wa familia yenu kushirikiana katika miradi mikubwa zaidi, kuonyesha thamani ya kila mmoja katika ndoa.
Nyumba ni zaidi ya makazi; ni mfano wa usalama, maono na mpango wa maisha. Kwa hekima, ujasiri na uwazi, unaweza kumshirikisha mume wako bila kuathiri ndoa huku ukilinda malengo yako ya kifedha na kuhakikisha kwamba nyumba hii inabaki kuwa uwekezaji wenye faida kwa siku zijazo.
Zingatia unapozungumza naye usimlaumu kwa kutojenga au kuwa mbishi kufanya hivyo, ila mwelimishe kuwa kujenga nyumba ni zaidi ya makazi ni uwekezaji pia. Ila siku nyingine usifanye jambo bila kumshirikisha mumeo, ninyi ni mwili mmoja.
