Tuwaandae watoto wa kiume kuja kuwa wanaume

Dar es Salaam. Katika jamii ya leo, tunashuhudia kizazi cha vijana wa kiume kinachokua bila mwelekeo wa kweli wa uanaume.

Wengi wao wamekosa misingi ya uwajibikaji, ujasiri na bidii kama nguzo muhimu zinazomfanya mwanaume awe nguzo ya familia na jamii.

Ni wakati sasa wazazi, walimu, na viongozi wa dini wafufue jukumu la kuwaandaa watoto wa kiume kuwa wanaume kamili, si vijana wanaosubiri kulelewa na wanawake wenye fedha.

Uanaume si suala la umri wala ukubwa wa misuli, bali ni uwezo wa kubeba majukumu. Mwanaume wa kweli ni yule anayesimama kama kiongozi wa familia, anayetafuta riziki kwa jasho lake na kulinda heshima ya nyumba yake.

Hata hivyo, tunazidi kuona vijana wengi wanaotegemea wake, wazazi, au wapenzi wao kifedha, wakibadilisha majukumu ya asili ya uanaume kuwa urahisi wa maisha.

 Ni aibu kuona vijana wakijivunia kuishi kwa pesa za wanawake badala ya kujivunia matunda ya kazi zao wenyewe.

Kizazi kipya kimepoteza dira kwa kufuata mitindo ya maisha ya starehe na anasa. Wengi wanashinda majimboni (gym) wakijenga miili mikubwa ya kuvutia mitandaoni badala ya kujenga maisha yao kwa kazi na maarifa.

Miili yenye nguvu haina maana kama haina akili, maadili, na wajibu. Badala ya kushindana kwa picha za “six pack”, vijana wanapaswa kushindana kwa kujenga biashara, kutafuta elimu, na kuweka akiba kwa ajili ya familia zao za baadaye.

Jamii inahitaji wanaume wanaojua maana ya kujituma, kutunza heshima ya wanawake, na kuwa mfano bora kwa watoto wao. Wazazi nao wana jukumu kubwa kuwafundisha watoto wa kiume kazi za mikono, kuwapa nidhamu, kuwafundisha kuheshimu muda na mali, na kuwapa maono ya kesho.

Mwanaume anayeandaliwa vizuri leo ndiye baba bora wa kesho, na ndio msingi wa taifa lenye maadili, maendeleo na umoja.

Uanaume si kulalamika, bali ni kuchukua hatua. Si kusubiri kusaidiwa, bali kusaidia wengine. Wakati umefika tubadili fikra na kuwekeza katika kuwalea wavulana kuwa wanaume wa kweli yaani wanaume wanaojituma, wanaoheshimu, wanaopenda familia zao, na wanaosimama kama nguzo imara za familia, jamii na taifa zima.