Sababu wanaume kukimbia kuoa warembo

Dar es Salaam. Ni ukweli kwamba wako wanawake wengi wanaoona kuwa kuzaliwa warembo ni baraka na neema ya kipekee.

Mara nyingi huzingatiwa kuwa watu wenye mvuto, wanaovutia macho ya wengi na wanaopewa nafasi ya kwanza katika makundi mbalimbali ya kijamii. Hata hivyo, pamoja na baraka hii ya uzuri unaoonekana kwa nje, uko upande mwingine wa simulizi ambao si wengi wanaouzungumzia waziwazi.

Kwa baadhi ya wanawake, uzuri wao umekuwa chanzo cha maumivu, upweke, kuumizwa hisia na hata kukatishwa tamaa katika safari ya kutafuta uhusiano wa kudumu na wenye kuheshimika.

Wanaume wengi wanapenda kuwa karibu na wanawake warembo, na hilo halina ubishi. Mara kwa mara, wanaume huonyesha hamu kubwa ya kuwafukuzia, kuwaongelesha, kuwapa sifa na hata kutamani kuwa nao kimapenzi. Lakini mara nyingi, nia hiyo si ya dhati kama inavyoonekana. Mwanaume huyo huyo anayemtongoza msichana mzuri kwa udi na uvumba, ndiye anayemchukulia kama chaguo la kupitisha muda, si chaguo la maisha. Ndiyo maana katika simulizi nyingi, utakuta msichana mrembo amekuwa na uhusiano wa muda mrefu na mwanaume fulani, akiamini kwa dhati kuwa mwisho wa safari ni ndoa.

Lakini ghafla, habari zinakuja kuwa huyo mwanaume ameoa, na aliyeolewa si yule mrembo aliyekuwa akijua “nafasi yake.” Hili limewaumiza wanawake wengi kiasi cha wengine kukata tamaa kabisa na uhusiano wenye maana.

Wapo walioamua kujirahisisha ili maisha yaendelee; wapo waliokubali kutunzwa na wanaume wenye ndoa; na wapo waliokubali kwamba “kuolewa si kwao.”

Msingi wa maamuzi haya mara nyingi hawajausimulia hadharani, lakini ni matokeo ya kujeruhiwa mara kwa mara katika safari yao ya mapenzi.

Tafiti na maelezo ya wataalam wa uhusiano yanaonyesha kuwa mwanamume akidumu kwa muda mrefu na mwanamke mrembo bila hatua ya kuelekea ndoa, kuna uwezekano mkubwa kuwa mwanaume huyo ni miongoni mwa makundi yanayoitwa players.

Wanaume hawa huona kuwa kuwa na mwanamke mzuri ni sifa ya kujiongezea heshima mbele ya wenzake. Lakini wanapofikiria kujenga familia na mwanamke huyo, mara moja huwapata woga.

Hata wanawake wenyewe wanajua mtazamo huu, na mara nyingi huwakejeli wanawake warembo wakisema, “mtachezewa tu na kuachwa.”

Ni jambo la kushangaza kuona hata wanawake wa kawaida wakitoa kauli hizi. Katika mabishano ya kimapenzi, binti wa kawaida humwambia mrembo, “we jifurahishe tu, lakini ujue huolewi.” Kauli hiyo inaonyesha namna imani hii imekita mizizi katika jamii.

Wanawake warembo wakiona hali hii inaendelea, huanza kuamini kuwa wanaume wote ni sawa: wanaume wa starehe tu, si wa kujenga familia. Wanaendelea kusubiri “mwanaume sahihi,” lakini muda unavyozidi kwenda, moyo unachoka.

Baadhi yao huanza kuwafukuzia wanaume wenyewe, jambo ambalo kwa bahati mbaya huwafanya wanaume wengi wahisi kutishika. Wanaume wanaamini kwamba wao ndio wanastahili kuwa wa kwanza kuonyesha nia, na mwanamke mzuri akiwa mbele akimtongoza mwanaume, mara nyingi huzua maswali kuliko majibu. Wengine huenda mbali na kusema, “kama mzuri kama huyu ananikimbiza, lazima ana tatizo.”

Kwa upande mwingine, uzuri wenyewe huwa kikwazo. Wanaume wanapokaribia, wanaanza kuona kuwa uzuri huo una gharama. Mara nyingi wanaume wa kipato cha kawaida huogopa kuwa hawawezi kumudu “mahitaji” yake.

Wengine wanakosoa kuwa uzuri mwingine ni wa “dukani,” hivyo hawana uhakika wanachokiona ni halisi au ni matokeo ya uwekezaji wa bidhaa mbalimbali za urembo.

Sababu mojawapo inayowafanya wanaume wahofu kuoa wanawake warembo ni hofu ya ushindani. Mwanaume anajiuliza: “Kama sasa hivi matajiri wanamfukuzia kama nyuki kwenye asali, itakuwaje nikiishi naye? Je, nitaweza kustahimili vishawishi vyote?”

Wengine wanaamini kuwa wanawake warembo wanavuta wanaume wengi sana, na hilo huongeza hofu ya usaliti ndani ya ndoa.

Lakini ukweli ni kwamba si wanawake wote warembo wana matatizo haya; si wanaume wote wana mtazamo huo; na si kila uhusiano unaishi kwa misingi ya imani hizi. Lakini ukweli mwingine ni kwamba imani hizi zimeenea sana katika jamii na mara nyingi huathiri jinsi wanaume wanavyowachukulia wanawake warembo katika suala la ndoa.

Kwa ujumla, sababu za wanaume kukimbia kuwaoa wanawake warembo ni mchanganyiko wa imani zilizojengeka kijamii, hofu ya usalama wa hisia, hofu ya kifedha, hisia za kutostahili, na wakati mwingine mitazamo potofu dhidi ya uzuri wenyewe. Wakati mwingine tatizo si uzuri, bali dhana ambazo jamii imezijenga kuuhusu uzuri huo.