BEKI raia wa Tanzania, Jackson Kasanzu anayekipiga Tormenta FC ya Marekani baada ya kuitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kitakachowania Fainali ya Mataifa ya Afrika (AFCON), kwake ni jambo la fahari.
Fainali hizo zitakazofanyika nchini Morocco kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026, timu ya taifa ya Tanzania itashiriki ikiwa ni mara ya nne baada ya 1980, 2019, 2023 na sasa 2025.
Kasanzu amesema: “Ni jambo la kumshukuru Mungu kwangu kuitwa Stars ilikuwa ndoto yangu niitumikie timu yangu siku moja hata hivyo inanipa motisha ya kupambana zaidi kwa kuwa nisiishie kuitwa tu bali nicheze pia.”
Huu ni msimu wake wa kwanza beki huyo anayesifika kwa kukaba kwa akili kuitumikia timu hiyo ambapo alikuwa nje ya uwanja kwa takribani msimu mzima akiuguza majeraha.
Beki huyo mwenye miaka 22 amekuwa na kiwango bora msimu huu akijiunga na chama hilo linaloshiriki Ligi Daraja la kwanza Marekani akitokea San Diego Loyal FC.
Kwa Marekani hadi sasa amezitumikia timu tatu, mwka 2022 alikuwa na AFC Ann Arbor akacheza mechi tisa, uliofuata akasajiliwa San Diego alipocheza mechi 19 za mashindano yote na sasa Tormenta.
