Siri ya Geita Gold ikisaka pointi 12

GEITA Gold inazidi kuchanja mbuga katika vita ya kupanda daraja kwenda Ligi Kuu msimu huu, huku ikiendelea kugawa vichapo kwa wapinzani na kutuma ujumbe kuwa imejipanga vyema kwa safari hiyo mpya.

Timu hiyo inaongoza Ligi ya Championship ikiwa na alama 22 katika michezo minane ikiwa imeshinda saba na sare moja ikifunga mabao 18 na kuruhusu mawili.

Inachuana kwa karibu na Kagera Sugar yenye pointi 22 zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Baada ya kukusanya alama zote 12 mwezi Novemba ikizifunga Hausung 3-0, African Sports 1-0, Gunners 3-0 na Polisi Tanzania 2-0, kikosi hicho kinazitaka alama zingine 12 katika mechi nne zijazo za mwezi Desemba, ambapo kwa Desemba hii timu hiyo itacheza ugenini dhidi ya Mbuni (Desemba 12) na TMA Stars (Desemba 16), kisha itazikaribisha Kagera Sugar na Ken Gold kwenye Uwanja wa Nyankumbu zitakazopigwa kati ya Desemba 21 na 27.

GEI 01

Nahodha wa zamani wa Tabora United, Said Mbatty anayekipiga Geita Gold kwa sasa, amesema siri ya kufanya vizuri ni kikosi kuwa tayari muda wowote, kwani kila mchezaji yuko sawa na kila mchezo ni kama fainali.

“Sisi ni timu ambayo ina malengo ya kutoka huku chini na kupanda daraja kwahiyo lazima kila mchezo tuwe na tahadhari nao tunajua wenzetu nao wanakuja kushindana, hivyo sisi tunatakiwa tushindane zaidi ya wao,” amesema Mbatty na kuongeza:

“Sisi tuna uhitaji wa alama tatu kila mchezo kuliko timu yoyote iliyo kwenye mashindano haya. Geita Gold malengo yetu ni kwenda Ligi Kuu ndiyo maana timu zinapokuja zinajaribu kutuwekea kizingiti, ili kutimiza malengo yetu tunaamini kila mechi kwetu ni fainali.”€

Kocha Mkuu wa Geita Gold, Zuberi Katwila amesema ligi hiyo ni ngumu na kila mpinzani anataka matokeo mazuri, lakini pointi walizokusanya mpaka sasa zinawapa mwelekeo na picha ya kwamba wao ni timu ya namna gani.

GEI 02

“Saikolojia ya wachezaji wangu iko sawa na haitakiwi iwe ya kujiamini kupita kiasi, lakini tunachotakiwa tu ni kuwa na ari na umakini katika kila mchezo,” amesema Katwila na kuongeza:

“Nawapongeza wachezaji wangu tumejenga mazoea ya kushinda na uoga wa kupoteza mechi umeondoka, kilichopo ni kushinikiza kuwalazimisha wapinzani wafanye makosa na kuyatumia.”