Mabula ataja sababu ya kutoanza vizuri Azerbaijan

KIUNGO wa Shamakhi FC, Alphonce Mabula ameeleza sababu za timu hiyo kutoanza vizuri katika Ligi Kuu Azerbaijan msimu huu, akitaja ugumu wa ligi hiyo na ushindani uliopandishwa na timu zinazoshiriki mashindano ya Ulaya.

Shamakhi imecheza mechi 13, ikishinda tatu, kutoka sare tano na kupoteza tano, rekodi ambayo imekuwa ikiwatia presha mashabiki.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mabula amesema kuwa kiwango cha ushindani kwenye ligi hiyo kimebadilika msimu huu, kutokana na timu kadhaa kuwa na uzoefu wa kucheza mashindano ya Ulaya, jambo linaloifanya ligi iwe na kasi na ugumu.

“Kwenye karatasi unaweza kuona ni ligi ndogo, lakini ukweli ni tofauti. Timu nyingi zinacheza Ulaya, zinakuja zikiwa na kasi kubwa, nguvu, nidhamu na uzoefu wa kimataifa. Sisi kama Shamakhi tumekuwa tukijitahidi, lakini ugumu wa ligi umekuwa sababu ya kutoanza vizuri,” amesema Mabula.

“Kama wachezaji tumekuwa tukipambana kuhakikisha tunaendana na kasi ya ligi. Tunajua mashabiki wanataka matokeo, na tumejiwekea malengo makubwa kwenye mzunguko wa pili.”

Mabula ambaye alijiunga na Shamakhi akitokea FK Spartak Subotica ya Ligi Kuu ya Serbia alikocheza kwa misimu miwili huu ni msimu wake wa pili ambapo hadi sasa amefunga bao moja.

Msimu uliopita kiungo huyo fundi alifunga mabao matatu kwenye mechi 17 alizocheza akiisaidia Shamakhi kumaliza nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi hiyo iliyokuwa inashirikisha timu 10 kwa sasa zimeongezeka timu mbili.