Arusha. Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Arusha, Flora Zelothe amewataka wanawake kuwa mstari wa mbele kulinda misingi ya amani na utulivu nchini, sambamba na kuwaelimisha vijana kuheshimu uhuru na uzalendo ulioasisiwa na viongozi wa awali.
Akizungumza jana, Jumamosi Desemba 6, 2025, katika Mkutano wa Baraza la UWT uliojadili mafanikio ya ushindi wa Rais, wabunge, madiwani na vurugu zilizojitokeza Oktoba 29, 2025, Zelothe amesema matukio hayo hayapaswi kurudiwa kwa kuwa yameacha majeraha na makovu mengi.
Amesema ushindi wa kishindo alioupata Rais Samia Suluhu Hassan ni kielelezo cha imani ya wananchi kwa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Hivyo, amesema baada ya uchaguzi ni wajibu wa wanawake kuliombea Taifa liwe na umoja, lisigawanywe kwa misingi ya itikadi za kisiasa.
“Mama ni amani. Uchaguzi umeisha, lakini tuna jukumu kubwa kwa imani zetu kulisihi Taifa libaki salama, na tumwombee Rais aiongoze nchi ifikie malengo ya Ilani ya CCM 2025–2030. Tusichoke kujibu matamshi yenye viashiria vya uvunjifu wa amani, hasa kwenye mitandao,” amesema Zelothe.
Pia, amesema baadhi ya matukio yaliyojitokeza kipindi cha uchaguzi yanaashiria kuwa, vijana wameachwa bila mwongozo, hivyo kuamua kudai haki kupitia maandamano yenye vurugu njia ambayo imeiacha nchi katika picha isiyofaa.
Amesisitiza kuwa, wanawake wanapaswa kuendelea kukaa na vijana wao na kuwafundisha njia sahihi, yenye kuzingatia uzalendo na kuepuka machafuko.
“Serikali imetambua umuhimu wa vijana, ndiyo maana imeteua waziri wa vijana kushughulikia changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi,” amesema.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wenyeviti na makatibu wa UWT kutoka wilaya zote saba za kichama pamoja na wabunge na madiwani wa viti maalumu. Washiriki hao pia walijadili umuhimu wa kuhakiki mali za umoja huo ili zitumike kuanzisha miradi ya kujipatia mapato.
Mbunge wa viti maalumu, Cecilia Paresso amesema yeye na wabunge wenzake wa UWT Arusha, Marirta Gido na Chiku Issa wamejipanga kutekeleza majukumu yao ya kibunge kwa ufanisi na kushirikiana na Serikali kuhakikisha ahadi ya Rais Samia ya kuwapa Watanzania tabasamu inatimia.
“Tuna jukumu la kuhakikisha ilani ya CCM inatekelezwa ndani ya mkoa na Taifa. Ilani yetu imejikita katika misingi ya kazi, utu na tunasonga pamoja. Rais aliahidi kuwa, akimaliza kipindi chake ataacha tabasamu, sisi tuna wajibu wa kulisaidia hilo kufanikiwa,” amesema Paresso.
Kwa upande wake, Chiku amewataka wanawake kuungana bila kujali nafasi zao ili kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM, inayojikita kwenye masuala kama afya, elimu na miundombinu pamoja na kuhakikisha sekta hizo zinatoa matokeo chanya kwa wananchi.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza misingi ya amani kuanzia ngazi ya familia, akiwataka viongozi wa UWT kuwa mfano kwa kuhubiri amani na kuonesha faida zake kwa jamii.
