Serikali yaahidi kutoa alama ya ubora zao la mwani

Unguja. Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Masoud Ali Mohammed, ameahidi kuwapatia wazalishaji wa bidhaa za mwani alama ya ubora na uthibitisho, ili kuongeza thamani ya bidhaa hizo na kuimarisha uaminifu katika soko.

Hayo amesema leo, Jumapili, Desemba 7, 2025, katika ziara ya kukagua miradi ya uchumi wa buluu na uvuvi katika Mkoa wa Kusini Pemba.

Waziri Masoud amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha sekta ya mwani na kuwawezesha wazalishaji kuongeza thamani ya bidhaa zao.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Masoud Ali Mohammed na Naibu wake Mboja Ramadhan Mshenga wakikagua eneo linalotarajiwa kujengwa kiwanda cha kukata mwani na majongoo bahari Pemba.

“Serikali inatambua thamani ya zao hilo kwa wakulima ndio maana inafanya juhudi mbalimbali ili kuongeza tija kwao,” amesema Masoud. 

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wakulima wa mwani wananufaika zaidi kupitia utafiti, teknolojia na sera zinazowawezesha kuongeza kipato chao.

Amesema kuwa mafanikio ya sekta hiyo yanategemea nidhamu, ubunifu na mshikamano. Hivyo, amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na miradi hiyo na kujikomboa kiuchumi.

Sambamba na hilo, amesema Zanzibar inahitaji mageuzi makubwa ya kiuchumi kupitia sekta ya uchumi wa buluu na uvuvi, hatua itakayoimarisha uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi. 

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Masoud Ali Mohammed na Naibu wake, Mboja Ramadhan Mshenga wakikagua zao za mwani katika ziara yao kisiwani Pemba.

Naibu waziri wa wizara hiyo, Mboja Ramadhan Mshenga ameweka mkazo kuimarisha miradi na taasisi za uchumi wa buluu ili manufaa yake yawanufaishe wananchi wote.

Mkulima wa mwani, Ali Mbrouk Juma, amesema bidhaa zao zinakosa ubora kutokana na vifaa vinavyoharibika wanavyotumia.

Amesema Serikali ndio walezi kwa wakulima wote, hivyo ni wakati sahihi kujipanga vizuri katika kuwainua wakulima wa zao hilo.