Dar es Salaam. Wakati kukiwa na vuguvugu la kufanyika kwa maandamano Desemba 9 2025, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir, amewaomba Watanzania waepuke kushiriki katika mpango huo.
Mufti Zubeir ametoa wito huo leo Jumapili Desemba 7 , jijini Dar es Salaam, alipokutana na viongozi wa taasisi mbalimbali za Kiislam, makao makuu ya Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata).
Amesema kwa wale wanaohamasisha kufanya fujo aidha siku hiyo ya Desemba 9 au siku zijazo, waache kwa kuwa hazina nia njema nchi na zitakapotokea vurugu hakuna atakayebaki salama.
“Nitumie fursa hii kuwaomba viongozi wa dini wakiwemo makatibu wa Kata, ngazi ya wilaya hadi mkoa kuendelea kuzungumza na wananchi wawe watulivu katika kipindi hiki.”
“Pia wahakikishe wanakuwa walinda amani na kuepuka kuwa wachochezi ambao unaweza kuwagawa na hii iwe popote kule ikiwemo kwenye mitandao ya kijamii,”amesema kiongozi huyo.
Kwa upande wa wazazi, Mufti huyo amewataka wawape nasaha vijana wao wasikubali kuingizwa kwenye mkumbo na wasioitakia mema nchi.
“Aidha kwa wale Watanzania walio nje ya nchi nao naomba waipende nchi yao badala ya kuiangamiza kwa kuwa kufanya hivyo ndio ukamilifu wa imani, na wasisahau kuwa nyumbani ni nyumbani,”amesema.
Amefafanua kuwa nchi itakapoharibika hasara zitakuwa kwa wote wakiwemo jamaa zao waliopo Tanzania.
Kwa viongozi wa Serikali amewataka kupokea kero za wananchi na kuzitatua kwa wakati ili kuepusha malalamiko yasiyo ya lazima.
Katika hatua nyingine Mufti huyo amewasihi viongozi wa dini kuacha kutoa matamko yanayoelekea kuwagawa Watanzania.
Amesema tangu kulipotokea vurugu hizo za Oktoba 29, viongozi mbalimbali wa dini wamekuwa wakitoa matamko kwa nyakati na maeneo tofauti ambayo mengine yanaonekana kabisa kuchangia kueneza chuki badala ya kulinganisha Taifa, jambo ambalo likiachwa liendelee litaipeleka nchi pabaya.
Amesema mafundisho ya Kiislam yanataka kila mwislam kuishi kwa kujiepusha na kila jambo litakalomletea madhara au kumletea mtu mwingine madhara.
“Maagizo ya Mwenyezi Mungu yanasema usijidhuru wala kukidhuru na ndivyo Mwislam anatakiwa kuishi na hii ni kwa aliye Mwislam na asiye.”
“Kwa msingi huu ni muhimu kwetu kuepuka upepo mbaya unaosambaa kwa kasi katika nchi yetu ya chuki za kidini jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa Taifa letu,”amesema Mufti Zubeir.
Pia Mufti Zuber amesema katika harakati za kuliponya Taifa kwa yaliyotokea, tayari Bakwata nao wameanza juhudi za kukutana na taasisi zingine za dini wakiwemo Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), ili kulirudisha Taifa katika hali yake.
Amesema hayo ni makubaliano waliofikia wakati walipotoa tamko lao la pili kuhusiana na sakata hilo kuwa ni vema kukutana na madhehebu mengine ili kujadiliana namna ya kulitoa Taifa katika mkwamo uliopo sasa.
“Tangu zilipotokea vurugu zile, tulitoa tamko la kwanza na la pili, ambapo katika hilo la tamko la pili tulilolifanya kwa kushirikiana na taasisi zote 25 zilizopo kwenye baraza tulikubaliana ni vema kufanya mazungumzo na madhehebu mengine,”amesema.
Amesema, “Niseme tayari kazi hiyo imeanza ambapo pia makatibu wakuu wa TEC na Bakwata wameshakutana mara kadhaa na hata sisi viongozi wakuu tumekutana na mazungumzo hayo yanaenda vizuri.”
“Naamini kwa kuwa lengo letu ni kuinusuru nchi yetu, na kurejesha taswira yake watu na mali zao, tutafanikiwa,” amesema kiongozi huyo wa dini.
