Dar es Salaam. Sherehe za harusi zinaendelea kuwa matukio ya kijamii yanayovutia umati na kuonekana kwenye mitandao ya kijamii. Hata hivyo, ibada ya ndoa, ambayo ni kiini cha tukio, imeonekana kuhudhuriwa na watu wachache ikilinganishwa na zamani.
Maendeleo ya teknolojia, vipaumbele vipya vya maisha, mizigo ya kiuchumi na mitazamo mipya ya uhusiano vinaibuliwa kama sababu muhimu za mwenendo huo.
Baadhi ya wadau wa masuala ya kijamii wakiwamo wazee, wanasema ongezeko la sherehe za kifahari limebadilisha uhusiano wa watu na ndoa.
Siku hizi watu wengi wanaonekana kuvutiwa zaidi na tukio la kijamii linalotoa burudani, muziki na upekee wa mapambo, kuliko ibada ya kiroho au hatua rasmi ya kuhalalisha ndoa.
Katika harusi za mjini, hali imekuwa ya wazi, ukumbi wa sherehe hufurika, lakini wakati wa kiapo cha ndoa kanisani au ofisi ya Serikali huwa tofuti.
Hili linatajwa na wazee kuwa linaondoa heshima na thamani ya ndoa, ukarimu na ushiriki wa jamii unaonekana kuhamia kwenye burudani badala ya kiini cha tukio.
Hali hii halisi imeibua mijadala kuhusu thamani ya sherehe na ndoa yenyewe, baadhi ya wazee na viongozi wa dini wanasema mabadiliko haya yanadhoofisha misingi ya familia.
Akizungumza hivi karibuni, mzee Deus Mwanyika kutoka Dar es Salaam, amesema mambo haya hayakuwepo zamani, lakini yanaibuliwa na vijana wa kizazi kipya wanaoiga maisha ya jamii za nje.
“Zamani harusi ilikuwa tukio kubwa tena linachukua siku kadhaa, na ndoa inafungwa siku linahitimishwa tukio hilo, lakini siku hizi sherehe na ndoa vimetenganishwa na watu wanataka sherehe zaidi kwenye ndoa hawaji,” amesema.
Amesema mwingiliano wa jamii kwa sasa, umekuwa mkubwa tofauti na zamani hali inayoathiri mila za Kitanzania na kuwa na jamii inayoishi kwa kuangalia wengine wanafanyaje.
Hata hivyo, viongozi wa dini nchini wameelezea wasiwasi mkubwa juu ya kuongezeka kwa tabia ya waumini kuhudhuria sherehe za harusi pekee, huku wakikwepa au kuchelewa kuhudhuria ibada maalumu ya ndoa inayofanyika kanisani au msikitini.
Wameitaja hali hiyo kuwa ni dalili ya kuporomoka kwa misingi ya kiimani na heshima ya sakramenti ya ndoa.
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Wolfgang Pisa amesema semina nyingi za ndoa ziwahamasishe wanandoa kukumbuka hilo.
“Linaweza kuwa tatizo kubwa katika jamii ya sasa tunaiasa jamii kuhudhuria ibada ya ndoa ni muhimu, lakini suala hili linalohusu mambo ya kichungaji, lina utofauti kati ya mahali na mahali,” amesema Pisa.
Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana nchini, Dk Maimbo Mndolwa amesema kuna badiliko kubwa katika ibada za ndoa hivi karibuni ikilinganishwa na miaka ya nyuma, huku akitaja uhamasishaji hafifu wa kuhudhuria sherehe za ndoa kuwa chanzo.
Pia, amesema suala hilo linaenda sambamba na kutokuwa na mafundisho katika jamii pamoja na gharama kubwa ambazo jamii inaingia kwenye sherehe za ndoa kama ukumbi, muziki, chakula na vinywaji, hivyo kuifanya jamii ione hivyo ndivyo vyenye thamani.
“Sasa kule kwenye kanisa wanaona ni bure na watu huwa wanafurahia zaidi wanapoona kuna kitu cha thamani.
“Tunafikiri kwanza ipo haja ya kuisaidia jamii kutambua umuhimu wa lile tendo la kanisani hata kwa mkuu wa wilaya, wafike mahali wanandoa wenyewe wasaidiwe jukumu la kualika watu kwenye ibada ni sawa na jukumu la kualika watu kwenye sherehe,” amesema.
Askofu Mndolwa amesisitiza wanandoa husika kuwa, liwe jukumu lao kuhamasisha jamii kwamba wanaanzia kanisani au kwa mkuu wa wilaya.
Akizungumza leo, Jumapili, Desemba 7, 2025, Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhani Kitogo, amesema waumini wengi wamekuwa wakipoteza maana na baraka za ibada ya ndoa kwa kuacha kushiriki kifungo halisi cha ndoa, kilicho na fadhila za kidini.
“Kuhudhuria ndoa inapofungwa, hasa msikitini, ndiko kunaleta thawabu na baraka kwa anayehudhuria. Kuenda ukumbini pekee ni kujifurahisha tu, lakini ibada ni tukio la ndoa linapofungwa,” amesema Sheikh Kitogo.
“Mtume Muhammad (S.A.W.) alihimiza ndoa zifungwe misikitini, kwa kuwa hapo ndipo panapofanyika ibada. Utamaduni wa kufungia ndoa majumbani au ukumbini uliletwa na watu wenyewe, lakini hauendani na msisitizo wa sunna.”
Amesema katika ndoa ya Kiislamu kuna sehemu mbili tofauti kifungo cha ndoa na walima, ambao ni mlo wa shukrani unaotolewa baada ya ndoa.
“Walima ni sadaka ya chakula iwe mbuzi, kondoo, ng’ombe au hata ngamia kwa ajili ya tukio la ndoa ambayo inamaanisha shukrani. Lakini kinachotangulia na chenye thamani kubwa ni ndoa yenyewe, si sherehe,” amesema Sheikh Kitogo.
Pia, amesema changamoto iliyopo ni watu kuipa sherehe uzito kuliko ibada, kisha kuacha kuhudhuria sehemu muhimu ya ndoa na kuishia kwenye sherehe pekee.
Sheikh Kitogo ameisihi jamii kuzingatia mafundisho sahihi na kurudi kwenye misingi ya dini ili kulinda utukufu wa ndoa.
“Wanandoa na ndugu zao wanapaswa kufahamu kuwa kwanza ni ndoa, kisha walima; siyo sherehe. Sherehe haiwezi kuonekana kuwa na thamani zaidi kuliko ibada,” amesema.
Ametoa wito kwa wazazi, vijana na viongozi wa dini kuhakikisha wanazingatia utaratibu wa Kiislamu ili ndoa ziendelee kuwa nguzo ya maadili na utulivu katika jamii.
Wakati viongozi wa dini wakiikosoa tabia ya watu kuhudhuria sherehe badala ya ibada ya ndoa, vijana wengi wanaonekana kuwa na mtazamo tofauti, wakitoa sababu zinazoeleza kwanini hali hiyo imeenea katika jamii ya sasa.
“Muda wa sherehe ndio rahisi kufika,” amesema Neema Kijungi mmoja wa vijana walio na ajira za mijini.
Baadhi ya vijana wamesema ratiba za kazi na msongamano wa shughuli mijini huwafanya washindwe kuhudhuria ibada ya ndoa inayofanyika mchana au asubuhi.
“Kazi zetu zinamalizika jioni. Kufika kanisani saa nne asubuhi ni ngumu, lakini ukumbi saa 12 jioni tunaenda,” amesema Neema.
Kundi jingine la vijana wamesema ibada za ndoa zinachukua muda mrefu na mara nyingi hazina ubunifu, zikilinganisha na sherehe ambazo zina burudani, muziki na mwingiliano wa kijamii.
“Kwetu sisi ‘vibe’ ya sherehe ni kubwa zaidi kuliko kukaa kanisani saa nzima,” amesema msichana mwenye umri wa miaka 24.
Vijana wanaotumia mitandao ya kijamii wanasema sherehe ni sehemu muhimu ya kupiga picha, kushiriki video na kuonekana na marafiki.
“Ukumbini ndiko kuna mwonekano, mapambo na vibes. Ndiyo sehemu unapata content,” amesema kijana mmoja wa Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Mtaalamu wa Saikolojia John Ambrose amesema hilo ni tatizo kubwa miongoni mwa jamii, akibainisha kwamba wapo ambao kwa sasa wanahudhuria kanisani au katika ibada ya ndoa kwa malipo.
Amesema kinachotokea kimesababishwa na mambo matatu akitaja saikolojia, hulka na tatu ni mkumbo.
“Kisaikolojia, kwa nini mtu afanye anachokifanya, lazima kuwepo na msukumo wa ndani kuna kitu ambacho kinaenda kupatikana, sasa huo uhitaji unaopatikana kuna changamoto kubwa iwe kinapatikana kitu fulani, chakula au ninywe na kustarehe,” amesema.
Ambrose amesema hilo limekwenda mbali mpaka kwenye timu ya mpira, inapocheza uwanjani lakini hakuna watu waliohudhuria, “nchi za wenzetu wao wamejielekeza kutibu saikolojia zao anapokwenda uwanjani anapumzisha akili, anafurahia, anaburudika na kupata matibabu ya akili.
“Kwetu sisi matibabu yetu nile, nishibe, nilewe kama hamna anakwambia hizi harusi za soda siji, lakini kuna harusi zingine zinafanyika mtu haendi sababu ni harusi za soda zinakuwa katika muundo wa namna hiyo, wapo wengine sababu ya muda anashindwa kujipanga kuhudhuria kote, lakini si sababu kwani hakikuwa kipaumbele chake kama kulikuwa na msukumo ndani yake angetenga muda.”
Akizungumzia kwenye muundo, Ambrose amesema mambo wanayofanya watu leo ndiyo yanavyotengeneza kesho, kwa maana hulka inazaliwa suala hilo linakuwa ni la kwako.
Amesema jamii nyingi zipo katika kusherehekea kiunganishi kikubwa ni pombe, ulevi kama harusi ya mtu ni soda basi lazima uone watu wanahesabika.
“Kinachowaweka watu pamoja ni chakula, vilevi na ile bondi inayotengenezeka na kiakili inasukumwa na kemikali ya ‘dopamine’, kuna kemikali inayotengeneza maumbile yetu ya nje, ukimwambia harusi akili yake inasukuma kumfanya akumbuke kuna kula, kunywa na kusherehekea,” amesema.
(Imeandikwa na Herieth Makwetta, Pawa Lufunga na Devotha Kihwelo)
