Dar es Salaam. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Alex Malasusa amemkemea matamko yenye lengo la kuigawa na kuchochea chuki kwenye jamii dhidi ya dini zao.
Akizungumza katika Ibada ya uzinduzi wa jengo la kuabudia KKKT Usharika wa Madale Bethel leo Desemba 7, 2025, Askofu Malasusa amewashukuru Watanzania kwa kuitikia wito wa kanisa wa maombi kwa ajili ya Taifa na kuwaombea walioguswa moja kwa moja na madhara ya Oktoba 29,2025.
“Ninawaomba Wakristo, hivi karibuni nimesikia mwili wangu ukatikisika sana, watu wameanza kunyoosheana vidole kwa dini, ndugu zangu kama kuna silaha mbaya na inateketeza jamii yeyote ni pale unapojiona dini yako au umefanya jambo kwa ajili ya dini, hebu tuyaache, tuone sisi ni watoto wa Mungu.”
“Mungu ameruhusu dini mbili, Ukristo na Uislamu sijui kwa nini, mimi ninapomuona mtu wa dini tofauti ninaimarika zaidi katika imani yangu, naomba kwa kila mtu iwe hivyo. Tusimpende mtu au kumchukia kwa sababu ya dini bali tumchukie shetani kutokana na uovu wake ambao unaingia ndani ya mtu,”amesema.
Askofu Malasusa amesema haijalishi mtu ana dini gani lakini akiingiliwa na pepo lazima atakuwa muovu, hivyo ni muhimu kupambana na muovu kuliko mtu kutokana na dini yake.
Akitolea mfano jengo alilozindua, Askofu Malasusa amesema wapo watu wa dini mbalimbali wameshiriki kulijenga na hata katika maisha ya kawaida, wenye dini tofauti wanakutana hivyo akawasihi Watanzania kuzidi kupendana kwa kuwa Mungu ameleta dini kwa lengo la upendo.
“Yeyote anayeleta udini anapaswa kuogopwa kama ukoma kwa sababu katika vita ya dini hakuna atakayeweza kushinda kwa haraka. Hata katika huduma zetu za kijamii tusiwabague watu kwa dini zao, tumuone mtu kwa utu wake na wala sio dini, mtu akikuletea mawazo ya dini mkatae, muepuke,”amesema.
