KOCHA Mkuu wa Transit Camp, Shadrack Nsajigwa amesema kucheza mechi tano ugenini msimu huu bila ya kupoteza ni ishara ya ukomavu kwa wachezaji wa timu hiyo, licha ya ushindani mkubwa wanaoupata kutoka kwa wapinzani mbalimbali.
Akizungumza na Mwanaspoti, nyota huyo wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Taifa Stars, amesema sio rahisi kucheza mechi tano kati ya nane ugenini na kutopoteza kwa sasa, ingawa ukomavu na jitihada za wachezaji ndio siri inayowabeba.
“Ukiangalia mechi zetu mbili za mwanzo tumeanza na washindani wetu wakubwa kwa maana ya Kagera Sugar na Geita Gold na zote tumepata sare, haikuwa rahisi kwetu ila tulicheza kwa nidhamu ambayo imetufikisha hapa tulipo,” amesema Nsajigwa.
Katika mechi tano za ugenini, Transit imeshinda mbili ambazo ni ya bao 1-0, dhidi ya TMA, (2-0) v African Sports, huku tatu ikitoka sare ya (0-0) v Kagera Sugar, (1-1), v Geita Gold na (1-1) kutoka kwa maafande wenzao wa Polisi Tanzania.
Kwa mechi tatu za nyumbani, kocha huyo aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Namungo ‘Wauaji wa Kusini’, ameshinda mbili ya (3-1) v Songea United na (1-0) v Bigman FC, huku akichapwa moja ya mabao 3-2, dhidi ya kikosi cha Mbeya Kwanza.
Nsajigwa amejiunga na kikosi hicho cha maafande akiwa ndiye kocha mkuu baada ya Emmanuel Mwijarubi aliyeifundisha msimu wa 2024-2025 kuondoka, huku uongozi ukionyesha matumaini makubwa kwake kutokana na uzoefu wake katika soka la Tanzania.
