Dube aing’arisha Yanga ikisogelea kileleni

BAADA ya kuanza kwa kusuasua katika Ligi Kuu Bara msimu huu, sasa Prince Dube amefunga mfululuzo baada ya leo Desemba 7, 2025 kuweka kambani bao moja lililoipa Yanga ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Union.

Dube amefunga bao hilo pekee dakika ya 87 kwa kichwa akiunganisha krosi ya Duke Abuya. Hiyo ilikuwa ni mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Pasi tatu zilipigwa katika kupatikana bao hilo baada ya Lassine Kouma kumuanzishia Pacome Zouzoua aliyempasia Duke ambaye aliuinua mpira uliomkuta Dube na kutikisa nyavu.

Kabla ya hapo, Dube alifunga bao moja Desemba 4, 2025 wakati Yanga ikishinda 2-0 dhidi ya Fountain Gate kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

YANG 02

Ushindi huo wa leo unaifanya Yanga kufikisha pointi 16 na kukamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikipanda kutoka ya tatu ilipokuwa awali na kuishusha Pamba Jiji.

Yanga imezidiwa pointi moja na JKT Tanzania, lakini pia imezidiwa mechi nne kwani JKT Tanzania imeshuka dimbani mara 10, huku Yanga ikiwa na sita.

Katika mechi sita ilizocheza Yanga msimu huu kwenye ligi, imeshinda tano na sare moja, imeendelea kuwa timu isiyopoteza sambamba na Azam.

YANG 01

Huu pia ulikuwa ushindi wa nne mfululizo tangu kikosi hicho kianze kufundishwa na kocha Pedro Goncalves ambaye pia ameiongoza Yanga kushinda mechi moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika na sare moja. Kocha huyo Mreno jumla amesimamia mechi sita, ameshinda tano na sare moja.

Baada ya mechi hii, Ligi Kuu Bara inasimama hadi Januari 21, 2026 ikipisha Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025) zitakazoanza Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026 nchini Morocco.