Serikali yatoa kauli maandamano ya Desemba 9

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene amesema kilichopangwa kufanyika nchi nzima Desemba 9, 2025 sio maandamano bali ni mapinduzi kwa kuwa  hayapo kisheria.

Amesema maandamano hayo yanayodaiwa hayana ukomo kufanyika nchi nzima ni kinyume cha sheria kwa kuwa hakuna ombi lolote la kimaandishi la kufanyika maandamano hayo, hakuna anayeratibu na wala hayajulikani yanaanzia wapi.

Kiongozi huyo amewasisitiza wananchi, Desemba 9, 2025 kama hakuna shughuli inayowafanya kutoka majumbani basi wakae nyumbani na wasishawishike kwa namna yeyote hata kuchungulia au kujitokeza kwenye maandamano hayo.

Msingi wa maelezo hayo ni kile kilichotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali nchini ambapo kulitokea maandamano yaliyozaa vurugu na kusababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa mali za watu binafsi na umma ikiwemo miundombinu ya majengo na usafiri.

Desemba 2, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam alisema kilichotokea Oktoba 29, 2025 kilikuwa ni kuipindua Serikali lakini walishindwa huku akisema wamejipanga vizuri kwa Desemba 9, 2025 na au wakati wowote.

Leo Jumatatu, Desemba 8, 2025, jijini Dar es Salaam, Waziri Simbachawene amekutana na waandishi wa habari akiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillus Wambura kuzungumzia hali ya usalama kuelekea Desemba 9.

Amesema Desemba 3, 2025, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa juu ya tishio lingine linalohamasishwa mtandaoni kwamba Desemba 9, 2025 kuna watu wanahamasisha na kupanga maandamano wanayoyaita yasiyo na ukomo, likisisitiza Serikali imeyazuia.

“Maandamano hayo hayaonekani yanaombwa na nani, yanaratibiwa na nani na madhumuni yake hayajulikani, maandamano yanayojulikana kisheria ni yale ambayo mtu anakwenda kuomba kibali na ujumbe unajulikana na Polisi wanafahamu.

Yale sio maandamano kwa kuwa hayana kibali, hayajulikani nani anafanya, hayo ni mapinduzi,” amesema.

Waziri huyo amesisitiza wote wanaoshabikia maandamano ya Desemba 9 na wanaoona wamechoka amani na watambue maandamano yaliyopangwa yapo kinyume cha sheria.

“Kama hukuna ulazima wa kutoka usitoke jizuie uone hali ikoje lakini uhakika uliopo upande wa Serikali na Jeshi la Polisi usalama utakuwepo kama unataka kutoka hatukuzuii lakini toka na vitu muhimu, na pia usichoke na maswali kwa sababu utaulizwa maswali,” amesema.

Kuhusu kuzimwa kwa mtandao, Simbachawene amesema wanaohamasisha maandamano hayo hutumia taarifa za taharuki mtandaoni, hivyo hadi sasa hakuna tishio lolote waliloona kama sababu ya kuzima mtandao na hata uzimaji wake kama utafanyika ni chaguo la mwisho.

Desemba 3, 2025 Msemaji wa Polisi, David Misime alisema maofisa wameona miito ya kufanyika maandamano katika mitandao ya kijamii, lakini akisisitiza hakuna hata mtu mmoja aliyetoa taarifa rasmi kwa polisi kuhusu kufanyika maandamano hayo.

Akizungumzia kuhusu ukamataji unaofanywa na Jeshi la Polisi, Waziri Simbachawene amesema tayari amefanya mazungumzo na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camillius Wambura ukamataji wa watuhumiwa uwe kwa mujibu wa sheria.

Aina ya ukamataji alioupinga Simbachawene, ni askari kuvaa kininja wakati wa kumkamata mtuhumiwa, kuwafuata majumbani watuhumiwa na silaha na kutovaa sare za jeshi la polisi.

“Ukamataji ninaoupenda mimi ni ule wa kisheria, askari anaenda anaripoti kwa mjumbe, mtu anajulikana yupo, kazini kwake wapi ya nini uende kumkamata nyumbani kwake umevaa kininja, tumekubaliana kwamba kuwe na ukamataji wenye staha,” amesema.

Amesema masuala ya kiusalama yapo mengi, pale inabidi mambo kama hayo yaendane na tukio lenyewe kuliko kakosa kadogo tu mtu kaposti kakitu tu, tumekubaliana mambo haya hayawezi kuwepo na nadhani baadhi ya mambo haya yanachochea wananchi kuchukia polisi,” amesema.