Dk Mwinyi azitaka taasisi kuacha muhali kukomesha ukatili wa kijinsia

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amezitaka taasisi zinazopinga ukatili wa kijinsia kuacha kuoneana muhali ili kukomesha vitendo hivyo vinavyoendelea nchini.

Amesema kuoneana muhali ni miongoni mwa sababu zinazochangia kukosekana kwa haki na utayari wa kupambana na janga hilo linalolitafuna Taifa.

Rais Mwinyi alisema hayo leo Jumatatu Desemba 8, 2025  katika hafla maalumu ya msimu wa tano wa tuzo za kupinga ukatili wa kijinsia, iliyofanyika Hoteli ya Madinat Al Bahr, Mbweni, mjini Unguja.

Amesema huu ni wakati sahihi kwa wadau kubadilika na kuwa tayari kuunganisha nguvu za pamoja kutokomeza tatizo hilo, kwa kuwa vitendo hivyo vina changamoto nyingi kwa waathirika.

“Ni wakati wenu wadau na taasisi zinazopinga ukatili wa kijinsia kuungana na kuongeza nguvu katika kupinga udhalilishaji na kuacha kuoneana muhali ili kukomesha vitendo hivi,” amesema Dk Mwinyi.

Pia, ametoa wito kwa jamii kutumia elimu na uzoefu uliopatikana katika siku 16 za kupinga udhalilishaji kuwa nyenzo ya kuongeza juhudi za kukabiliana na ukatili wa kijinsia.

Sambasamba na hilo, ameipongeza Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (Zafela), kwa kupinga vitendo hivyo akiahidi Serikali kuendelea kushirikiana nao.

Pia, ametoa wito kwa wadau na washirika wa maendeleo kuendelea kuiunga mkono Zafela kwa misaada na vifaa ili harakati za kupinga udhalilishaji ziwe endelevu na zenye mafanikio.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Anna Athanas Paul amesisitiza kuchukuliwa hatua mapema kupinga ukatili wa kijinsia ili kurejesha maadili ya Kizanzibari.

Mkurugenzi wa Zafela, Jamila Mahmoud, amesema taasisi hiyo imekuwa na utaratibu wa kila mwaka kuwatambua na kuwaenzi watu wanaotoa mchango mkubwa kwa jamii katika kupinga ukatili wa kijinsia.

Amesema, bado kuna tatizo kubwa la ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto, kwa kuwa taasisi hiyo imekuwa ikipokea wanawake takribani 10 kila siku wanaofikisha malalamiko ya kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji.

Katika hafla hiyo Rais Mwinyi ametunukiwa tuzo maalumu iliyotolewa na jumuiya hiyo kwa kutambua mchango wake  katika kuhakikisha masuala ya ukatili wa kijinsia yanaondoka Zanzibar.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,  kwa miezi mitatu kuanzia Agosti  hadi Oktoba, matukio 321 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa, waathirika wengi ni wanawake na watoto.

Agosti yalikuwa matukio 116 yaliripotiwa, watoto walikuwa asilimia 89.7 na wanawake asilimia 7.8.

Idadi ya matukio kwa mwezi huo yameongezeka kwa asilimia 8.4.

Pia, Septemba, matukio 106 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa, watoto walikuwa asilimia 88.7 wakifuatiwa na wanawake asilimia 11.3, idadi ya matukio kwa mwezi yamepungua kwa asilimia 8.6.

Oktoba, matukio 99 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa; watoto walikuwa asilimia 92.9 wakifuatiwa na wanawake asilimia 7.1. Idadi ya matukio kwa mwezi yamepungua kwa asilimia 6.6.