Baada ya furaha, abiria waacha vilio Magufuli

Dar es Salaam. Kati ya Novemba 30 hadi Desemba 7, mwaka huu zilikuwa siku za neema kwa wafanyabiashara kwenye stanedi kuu ya mabasi ya Magufuli, jijini Dar es Salaam kutokana na utitiri wa abiria waliokuwa wakisafiri kwenda mikoani.

Idadi kubwa ya abiria ilikuwa neema kwa wenye mabasi na wafanyabiashara ndogondogo waliopo ndani na nje ya kituo hicho maarufu kwa usafirishaji nchini.

Biashara zilichangamka kutokana na abiria waliokuwa wakisubiri usafiri kutumia muda mrefu ndani ya kituo hicho hivyo, ilikuwa neema kwa mama ntilie na wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali kwani, walikuwa wakipiga pesa.

Hata hivyo, leo Desemba 8, 2025 mambo yamekuwa tofauti na vilio vimeanza kusikika miongoni mwa wafanyabiashara kwenye kituo hicho wakiwemo wenye mabasi kutokana na abiria kupungua.

Kwa mujibu wa wafanyabiashara wadogo wanaojipatia kipato katika stendi hiyo, shughuli zimeanza kudorora tangu jana Jumapili, Desemba 7, 2025, hali waliyosema imewaacha katika kipindi kigumu, tofauti na wiki iliyotangulia ambapo biashara ilikuwa ikiimarika kutokana na wingi wa abiria waliokuwa wakikesha hapo kusubiri usafiri kwenda mikoani.

Hata hivyo, Meneja wa Stendi ya Magufuli, Isaac Kasebo, amesema kupungua kwa abiria katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka ni hali ya kawaida na si ishara ya changamoto zozote ndani ya kituo hicho, kama baadhi ya taarifa zinavyodai kwenye mitandao ya kijamii.

Akizungumza na Mwananchi, Kasebo amesema mabadiliko ya mwamko wa wasafiri katika stendi hiyo hutokea kila mwaka kutokana na misimu tofauti ya safari.

“Ni kawaida katika kituo chetu watu kuongezeka na kupungua hasa kipindi hiki cha mwisho wa mwaka. Kuanzia Desemba mosi hadi Desemba 7 kulikuwa na ongezeko kubwa la abiria, jambo lililochangiwa na shule nyingi kufunga,” amesema.

Kati ya Novemba 30 hadi Desemba 7, kulikuwa na hekaheka ya msongamano wa abiria waliokuwa wakisaka usafiri kwenda mikoani kwa sababu kuu tatu, baadhi walidai kwenda kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka, wengine walihofia usalama wao kutokana na uwezekano wa kuwapo maandamano yanayotarajiwa kufanyika kesho, na baadhi wakidai hali ya joto jijini Dar es Salaam limezidi, hivyo wanatafuta maeneo yenye unafuu kwa muda.

Wakizungumza leo Jumatatu, Desemba 8, 2025, na Mwananchi, baadhi ya wafanyabiashara katika stendi hiyo wamesema kitendo cha kukosekana kwa abiria kama ilivyo kawaida yake kumeathiri moja kwa moja vipato vyao walivyokuwa wakitegemee kuingiza kila uchwao.

Mfanyabiashara wa vitafunwa, Vedastus Tarimo, amesema kuwa matarajio yao yalikuwa ni kuona safari za mabasi zikiendelea kama kawaida, lakini hali imekuwa tofauti baada ya wamiliki wengi wa mabasi kusitisha safari na kuyaegesha.

“Tulitegemea mabosi wa mabasi wangeendelea kutoa safari, lakini wengi wamegoma na kupaki magari Shekilango. Hali hiyo imetuacha bila wateja, biashara inazidi kuwa ngumu kila siku,” amesema mfanyabiashara mmoja.

Felister Mgimba amesema kwa sasa wanahangaika kutafuta angalau Sh2,000 kwa mchana ili kufikisha Sh10,000 jioni, fedha ambazo hazitoshelezi mahitaji yao ya kila siku.

Mgimba, ambaye ni mfanyabiashara wa juisi na maandazi, amesema hali waliyonayo imewafanya kuishi kwa hofu, hasa kutokana na sintofahamu ya siku zijazo kuhusu taarifa za uwezekano wa maandamano yasiyo na ukomo.

“Nikuambie, hata kilichotokea Oktoba 29 kilitutesa. Mazingira yalikuwa magumu zaidi. Sasa hivi tunahangaika kutafuta Sh2,000 tu. Tunamuomba Mungu kesho ipite salama,” amesema.

Richard Ndomba, mfanyabiashara wa redio na ‘headphone’ katika stendi hiyo, amesema biashara imekuwa ngumu huku akisema anafikiria kusitisha shughuli zake kwa muda hadi hali itakaporejea kawaida.

Ismail Mgunda, anayefanya shughuli ya ubebaji mizigo ya abiria, amesema maisha yamekuwa magumu kwani katika kampuni yao, kupata chochote baada ya kazi inategemea kiwango cha mapato wanachoyaingiza kwa siku.

“Tangu asubuhi hadi sasa (mchana) sijapata kazi, na sijui itakuwaje, mtu mzima nina familia nyumbani, narudi bila chochote. Ni aibu. Tunaomba amani na kuwawezesha mambo yarejee kawaida,” amesema.

Siku kadhaa zilizopita, Stendi ya Magufuli ilikuwa na hekaheka za abiria waliokuwa wakihangaika kusaka usafiri kuelekea mikoa mbalimbali tangu Novemba 30.

Wingi wa watu na mtiririko wa mabasi uliifanya stendi hiyo kuwa kitovu cha shughuli za kila siku, huku wafanyabiashara wakinufaika na mahitaji ya abiria waliokuwa wakisubiri safari.

Hata hivyo, hali imegeuka ghafla. Sasa stendi ipo tulivu, hakuna msongamano wa abiria, na mabasi yanaingia moja baada ya muda fulani. Ndani, hakuna abiria.

Wengi wao wamesema hawana matumaini kama hali itarejea kawaida mapema, huku wakitoa wito kwa mamlaka husika kuhakikisha usalama ili shughuli zao zirejee na wao wapate riziki.

Uongozi wa Standi watoa hofu

Meneja wa Stendi ya Magufuli, Isaac Kasebo, amesema kupungua kwa abiria katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka ni hali ya kawaida na si ishara ya changamoto zozote ndani ya kituo hicho.

Akizungumza na Mwananchi, Kasebo amesema mabadiliko ya mwamko wa wasafiri katika stendi hiyo hutokea kila mwaka kutokana na misimu tofauti ya safari.

Amebainisha kuwa wazazi wengi walikuwa wakiwarudisha watoto nyumbani, huku wengine wakisafiri kuelekea mikoani kwa ajili ya maandalizi ya sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya.

“Matarajio yetu ni kwamba kuanzia Desemba 15 na kuendelea, hali itarejea katika kawaida yake kwa kuwa na abiria wengi,” amesema.

Kasebo amesema kupungua kwa abiria ni sehemu ya mzunguko wa kawaida wa shughuli za usafiri, akifafanua kuwa kipindi cha mwisho wa mwaka huwa na “low season” na “high season,” ambayo huathiri pia mzunguko wa wafanyabiashara wanaorudi mikoani kusherehekea sikukuu.

Ingawa amekanusha taarifa zinazosambaa mtandaoni kwamba stendi hiyo inatarajiwa kufungwa, amesema: “Hakuna utaratibu wa kufungwa kwa kituo. Huduma zinaendelea kama kawaida, na watumishi wanaonekana ofisini wakitekeleza majukumu yao. Kama kutakuwa na utaratibu wa kufunga, tutatoa taarifa kwa umma.”

Amesisitiza kuwa abiria wanaohitaji kusafiri wanapaswa kununua tiketi kupitia mtandao au kwenye ofisi rasmi za mabasi, ili kuepuka matapeli na watu wasiokuwa waaminifu.