Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema kuzimwa kwa mtandao wa intaneti ni hatua ya mwisho kabisa ambayo inaweza kuchukuliwa tu endapo hali ya kiusalama itakuwa mbaya kwa kiwango cha kutishia ustawi wa Taifa. Amebainisha kuwa hadi sasa, Tanzania ipo katika utulivu na hakuna tishio lolote linaloweza kuilazimisha Serikali au Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzima intaneti kesho, Desemba 9, 2025.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Desemba 8, 2025, Simbachawene amesema mijadala na taarifa za taharuki zinazozagaa mtandaoni hazijafikia kiwango cha kuhatarisha usalama wa nchi, licha ya kutumiwa na baadhi ya wanaharakati kusambaza taarifa zinazoweza kuleta mkanganyiko kwa wananchi.
“Kuhusu kuzimwa mtandao, kwa sababu nyenzo kubwa inayotumika na hawa wanaharakati wa mitandaoni ni taarifa za taharuki. Wengine wanapata shida wakisikia, wengine wanazifurahia. Mpaka sasa hatujaona tishio lolote la kutufanya tufikie hatua ya kusema mtandao umekuwa tatizo,” amesema Simbachawene.
Kauli ya Simbachawene imekuja wakati Watanzania bado wanakumbuka siku sita za kuishi bila kuwapo kwa mtandao wa intaneti.
Oktoba 29, baada ya kutokea maandamano yaliyosababisha vurugu mtandao wa intaneti nchini ulitoweka na kurudi katika hali ya kawaida Novemba tatu.
Akizungumza Simbachawene amefafanua kuwa intaneti ndiyo uti wa mgongo wa shughuli muhimu za kijamii na kiuchumi nchini, zikiwemo huduma za benki, usafiri na mifumo mingine ya kitaifa. Kwa msingi huo, Serikali haiwezi kuchukua hatua ya kuzima intaneti bila sababu nzito na ya kiusalama.
“Mtandao unatumika kutoa huduma nyingi za kijamii benki, usafiri na mengine. Kuzima intaneti ni chaguo la mwisho sana pale ambapo hali itakuwa mbaya. Hata kama sekta nyingine zina mamlaka ya kutoa maamuzi hayo, kwa upande wetu tunaona hali ni shwari. Hakuna tishio la kuifanya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), izime mtandao,” amesema Simbachawene.
