Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa ameziagiza hospitali zote nchini kuanza rasmi utekelezaji wa agizo la kutozuia maiti, huku akitoa maagizo kwa viongozi wa hospitali na taasisi zilizo chini ya wizara yake.
Amesema hakuna Mtanzania atakayeshindwa kutibiwa kwa sababu ya kukosa fedha, wala ndugu watakaonyimwa mwili wa mpendwa wao kwenda kuzika.
Mchengerwa amesema hayo leo Jumatatu, Desemba 8, 2025 wakati wa kikao kazi na watumishi wa sekta ya afya Mkoa wa Dar es Salaam kilichofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
“Sitegemei baada ya leo kusikia hospitali yoyote watu wameshindwa kwenda kuzika kwa sababu ya kuzuiwa maiti. Tumelizungumza hili mara kadhaa lakini utekelezaji wake umekuwa ukisuasua. Hospitali tafuteni vyanzo vya mapato ili kuondokana na hii changamoto,” amesema Mchengerwa.
Amesema suala la zuio la maiti lipo kwenye ahadi za siku 100 madarakani za Rais Samia Suluhu Hassan alizowaahidi wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Novemba 14, 2025, Rais Samia alizindua Bunge la Tanzania huku akitoa maagizo kwa Wizara ya Afya kusimamia maelekezo ya kutozuiwa maiti kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, wakati familia zikiendelea na taratibu za kulipa deni la matibabu kwa njia zinazolinda utu wao.
“Niseme kwamba, ni kupitia mpango huu wa bima ya afya, kadhia hii inakwenda kukomeshwa. Kwa sababu gharama za matibabu zitalipwa na bima ya anayetibiwa. Niwasihi wananchi wote kuweka kipaumbele kwa afya zetu, kwa kila mmoja wetu kuwa na bima ya afya pamoja na wanaomtegemea,” alisema Rais Samia.
Matukio ya kuzuiwa kwa miili yamekuwa yakitokea licha ya maelekezo na waraka mbalimbali kutolewa na viongozi wa Serikali, wakitaka hospitali, hasa za umma, zisizuie maiti kwa ndugu na jamaa wasio na uwezo wa kulipa gharama za matibabu.
Sio hivyo tu, suala hilo liliendelea kutokea hata baada ya Serikali kutoa Waraka Namba Moja wa mwaka 2021 wa kutozuia maiti na kuweka utaratibu wa kulipa gharama za matibabu na madeni kwa miili.
Kwa mujibu wa kifungu cha 3.1.4 cha waraka huo, iwapo ndugu wa marehemu hawatakuwa na uwezo wa kulipa deni pale mgonjwa atakapokuwa amefariki dunia, ndugu wataingia makubaliano ya maandishi na kituo cha kutolea huduma kuhusu namna ya kulipa deni na waruhusiwe kuchukua mwili.
Kutokana na hilo, Waziri Mchengerwa amesema kila hospitali na vituo vya afya viangalie utaratibu wa kushughulika na suala hilo ili lisijitokeze tena.
Pia, amekemea baadhi ya hospitali kuwa na tuhuma za kukaa na wagonjwa kwa muda mrefu bila kutibiwa.
“Naomba tujirekebishe kesi za aina hii nimezisikia. Maeneo mengine nimesikia ni vigumu kuwapata mabingwa na madaktari tarajali, baadhi yao si waaminifu wamekuwa wakiomba rushwa kwa wagonjwa ili wapatiwe huduma au kupangiwa tarehe za karibu za upasuaji, vitendo hivi sitaki kuvisikia, tuangalie mienendo yao,” amesema.
Pia, amegusia baadhi ya wagonjwa kusubiri vipimo kwa muda mrefu, akitolea mfano Taasisi ya Saratani Ocean Road kukaa na mashine ya Pet CT-Scan kwa muda mrefu bila kuitumia.
“Mashine hii hamjaanza kutumia mnasuburi uzinduzi, wagonjwa wanakaa muda mrefu bila kupata huduma, hamuwaambii ukweli mnawaingiza kwenye mchakato mwingine. Naagiza mashine hii ianze kufanya kazi si lazima waziri ndiyo aizindue,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mchengerwa ameshangazwa na Taasisi ya Mifupa (Moi) kukaa miezi miwili mashine tatu zikiwa zimeharibika bila matengenezo.
Amesema kuharibika kwa mashine hizo kumesababisha wagonjwa kukosa huduma.
“Moi mna makusanyo, viongozi mnashindwa kuidhinisha fedha mashine zikatengenezwe? Taarifa nilizonazo mashine ya Angio-Suite, CT-Scan, MRI zimeharibika miezi miwili sasa, viongozi mpo mashine zimeharibika, wengi ni marafiki zangu hapa lakini katika hili hapana, hii si staili yangu ya kufanya kazi,” amesema.
Pia, amemuelekeza katibu mkuu kufuatilia hilo, akisisitiza mashine hiyo yenye kazi ya upasuaji wa ubongo pasipo kufungua fuvu, lazima itengamae ili wagonjwa waendelee na matibabu.
“Nimepata pia taarifa kuna mashine hapa iliharibika kwa uzembe wa wataalamu…natoa wiki mbili, naomba nipate taarifa ya uchunguzi kuhusu hili,” amesisitiza.
Mchengerwa amesema atapita taasisi zote zilizo chini ya wizara yake na huenda kwingine akapita usiku, ikiwamo kwenye hospitali za mikoa na kanda.
Amesema ili kukabiliana na changamoto zinazowapata wagonjwa, atazindua mfumo wa wananchi kuzungumza naye kuhusu utendaji na atakuwa na ratiba ya kuzungumza na Watanzania kuhusu sekta ya afya, mfumo utakaokuwa tayari wiki moja kuanzia sasa.
Amesema miongoni mwa malalamiko ni kukosekana kwa dawa, hivyo aliagiza Bohari ya Dawa (MSD) kuweka mifumo ya kufuatilia dawa ili kuwapo na huduma hiyo kwa mwendelezo.
Akizungumzia Hospitali ya Muhimbili, Mchengerwa amemuagiza mkurugenzi wake, Dk Delila Kimambo kuhakikisha anawalipa fidia wafanyakazi waliohusika na kuokoa maisha ya Watanzania waliokuwa wagonjwa kipindi cha Oktoba 29, 2025.
“Nimeambiwa wengine mlikaa wiki nzima bila kurejea nyumbani. Kila aliyekuja hapa alihudumiwa bila kujali amekuja na nini, huu ni moyo wa kipekee. Waharakishie haki yao ya msingi, watumishi hawa waliokesha usiku na mchana si Muhimbili pekee; hospitali zote walipwe kama ambavyo Rais Samia amenielekeza niwaelekeze,” amesema.
Pia, ameiagiza Hospitali ya Taifa Muhimbili kuhakikisha inakuwa na viwango na ubora kwa kuwa na ithibati ya kimataifa.
Akizungumzia maboresho ya hospitali hiyo, Mchengerwa ametaka Muhimbili iwe mfano kusaidia maboresho katika hospitali zingine.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Dk Delila Kimambo amesema wanaadhimisha miaka 120 tangu kuanzishwa kwake na hospitali imeendelea kuimarika hadi kuwa taasisi ya kisasa.
Dk Kimambo amesema hospitali hiyo ilianzishwa mwaka 1905 ikiitwa Hospitali ya Sewahaji.
Mwaka 1956 ilijulikana kama Princess Margaret na mwaka 1976 Shirika la Afya Muhimbili na mwaka 2000 ilipandishwa cheo na hadhi na kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Chuo Kikuu cha Afya Shirikishi (Muhas).
Dk Kimambo amesema taasisi tatu za ubora zilizalishwa ikiwamo Taasisi ya Saratani Ocean Road, Moi na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
“Hospitali hii ina jumla ya vitanda 1,435 vilivyopo Muhimbili-Upanga na 608 Mloganzila. Tuna wafanyakazi jumla 4,070 kati ya hao 1,034 wapo Mloganzila wanaotoa huduma katika klikini 127 kila siku,” amesema.
Pia, amesema idadi ya operesheni zinazofanyika zimeendelea kupungua kutokana na kuboreshwa kwa miundombinu katika hospitali za kanda, zimepunguza mzigo mkubwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Ellen Senkoro-Mkondya alisema katika maadhimisho hayo ya kihistoria, hospitali imejipanga kuwa na matukio mbalimbali ikiwamo uendeshaji wa kliniki maeneo mbalimbali nchini (huduma mkoba), midahalo na utoaji wa huduma mbalimbali za kibingwa na bobezi.
“Mengine ni maboresho ya hospitali yatakayogharimu Sh1.3 trilioni, kuanzishwa kituo cha biashara buguruni kama kitega uchumi cha hospitali, kituo cha tiba kazi na kuongeza wigo wa mapato mengine kwa kuangalia hawatamuumiza mwananchi katika upatikanaji wa huduma,” amesema.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe amesema bajeti ya afya kwa jumla na taasisi zake imepanda pia kutoka Sh2.6 trilioni kwa mwaka 2024/25 na kwa sasa ni Sh3.1 trilioni.
Amesema ongezeko hilo limelenga kuboresha huduma za afya kuelekea bima ya afya kwa wote.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametoa shukrani kwa Rais Samia kuweka fedha nyingi katika eneo la afya huku akisema wamepokea Sh117 bilioni kwa ajili ya kushughulikia afya.
Pia, amesema watahakikisha huduma zinaendelea kupatikana bila changamoto yoyote
