Serikali yapiga marufuku askari wa majiji kuwanyang’anya wafanyabiashara bidhaa zao

Dodoma. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameyaagiza majiji yote nchini kuacha mara moja vitendo vya kuwanyang’anya wafanyabiashara wadogo bidhaa zao wanazouza mitaani, kwani ndiyo ofisi na mitaji yao ya kujikomboa kimaisha.

Aidha ameagiza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kufanya tathmini ya wafanyabiashara waliopo  kwenye masoko ya jiji hilo na kama bado kuna uhitaji watafute maeneo mengine ya kujenga masoko mapya na kuwaweka wafanyabiashara hao.

Dk Mwigulu ameyasema hayo leo Jumatatu Desemba 8, 2025 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Machinga Complex lililopo jijini Dodoma ili kujua kero zao.

Mmoja wa wafanyabiashara wa soko hilo, Richard Joseph alimweleza kuwa alinyang’anywa biashara yake na mgambo ya Jiji la Dodoma yenye thamani ya Sh420,000 pamoja na toroli alilokuwa amebebea bidhaa hizo, lakini pamoja na kufuatilia hajazipata mpaka leo.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu nimefuatilia bidhaa zangu kwa zaidi ya mara 20 lakini kila nikifika ofisi za Jiji nazungushwa tu na mara ya  mwisho nimeambiwa kuwa bidhaa zangu hazipo, mimi ni mfanyabiashara na pia ni msomi ambaye nimeamua kujiajiri kutokana na mfumo wa ajira kutoruhusu kila mtu aajiriwe lakini hata kwa hiki kidogo ninachokitegemea nacho wamechukua.

“Hata kama nilifanya kosa najua zipo faini za kulipa nimekwenda pale na faini yangu mkononi nawaambia nilipe ili wanipe mzigo wangu lakini jibu la mwisho nililopewa ni kwamba mzigo wangu haupo, kwa hiyo nakuomba Waziri Mkuu unisaidie kupata bidhaa zangu maana ndiyo mtaji wangu.”

Amesema alilazimika kwenda kuuza bidhaa zake kwenye eneo lenye mkusanyiko mkubwa wa watu kwa sababu soko la Machinga lina muda maalumu wa kufungua kulingana na aina ya wateja walionao, hivyo mgambo wa jiji walimnyang’anya bidhaa zake saa 2:40 asubuhi ambazo hajazipata mpaka leo.

Baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Waziri Mkuu aliyaagiza majiji yote nchini kuacha mara moja tabia ya kuwanyang’anya wafanyabiashara wadogo bidhaa zao kwani ndiyo ofisi yao na mitaji yao.

“Msichukue bidhaa za raia kwani hizo bidhaa ndiyo ofisi zao na ndiyo mitaji yao hata kama kuna jambo linalotaka kuelekeza au utaratibu ufanyike lakini bila kuchukua bidhaa za raia. Suala la kuchukua bidhaa zao halikubaliki,” amesema Dk Mwigulu.

Kuhusu bidhaa za mfanyabiashara huyo kupotea Waziri Mkuu ameagiza wahusika waliochukua bidhaa hizo wazirudishe na kama kweli zimepotea basi wahesabiwe ni wezi kama ilivyo kwa wezi wengine.

Pia ameagiza kufanyika kwa tathmini ya wafanyabiashara walioko kwenye masoko ya Jiji la Dodoma ili kujua kama kuna uhitaji wa kuongeza ujenzi wa masoko mengine ili kukidhi mahitaji ya wafanyabiashara.

Ameagiza wafanyabiashara ambao tayari wana vizimba kwenye masoko wasiondolewe bali wale ambao wanauhitaji watatafutiwa masoko mengine ya kwenda ikibidi kujengewa masoko mapya, ili kuepusha msongamano na vyanzo vya rushwa.

Ametoa kauli hiyo baada ya mfanyabiashara mmoja ambaye hakutaja jina lake kulalamika kuwa wameambiwa wataondolewa kwenye vizimba vyao, ili kupisha wafanyabiashara wengine waingie sokoni hapo.

Waziri Mkuu ameagiza asiondolewe mfanyabiashara yeyote kwenye kizimba chake, badala yake wenye uhitaji watatafutiwa maeneo mengine ya kwenda kufanya biashara.