MSHAMBULIAJI Prince Dube aliwafaa tena Yanga juzi baada ya kufunga bao pekee katika ushindi wa ugenini wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, lakini kocha wa timu hiyo, Pedro Goncalves amesimulia namna walivyopambana kumrudisha mchezoni Mzimbabwe huyo.
Yanga ilipata ushindi huo usiku kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kwa bao la dakika ya 88 kupitia Dube ambalo linakuwa la pili mfululizo baada ya lile la penalti ya mechi iliyopita dhidi ya Fountain Gate ambapo Yanga ilishinda 2-0, ilhali bao jingine likifungwa na Pacome Zouzoua.
Akizungumza na Mwanaspoti, Pedro alisema hatua ya Dube kuanza kufunga ni furaha ya kila mmoja katika kikosi chao ambapo wakati anatua kuanza kazi, mshambuliaji huyo hakuwa kwenye hali nzuri kuweza kufanya mambo makubwa uwanjani.
Pedro alisema Dube alikuwa hayupo sawa kisaikolojia hali ambayo ilimnyima nafasi ya kujiamini uwanjani na kushindwa kutekeleza majukumu yake vizuri hususan kufunga mabao kama anavyotakiwa.
Kocha huyo alisema baada ya kugundua hilo walianza kufanya kazi ya kumrudishia uwezo wa kujiamini na pia wakifanya naye vikao tofauti huku wachezaji wenzake wakiendelea wakimtia moyo kuamini kuwa anaweza kurudisha makali yake.
Tangu Pedro akabidhiwe kikosi cha Yanga, Dube ameshafunga mabao matatu na yote yameipa ushindi timuhiyo akianza na AS FAR Rabat katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kisha dhidi ya Fountain na juzi dhidi ya Coastal Union.
“Wakati tunafika hapa kila mmoja atakumbuka Dube hakuwa katika ubora wa kuweza kufanya kazi sawasawa. Unajua kufunga mabao unahitaji wakati mwingine mshambuliaji aweze kujiamini kwamba anaweza kufanya kitu,” alisema Pedro ma kuongeza:
“Kuna kazi imefanyika kuhakikisha anakuwa sawa. Tuliijenga saikolojia yake, lakini wachezaji wenzake nao walikuwa na msaada mkubwa, walikuwa wanazungumza naye na kumpa imani kwamba atarudi kwenye ubora wake.
“Nafikiri sasa anameanza kukaa sawa. Anafanya mambo yake uwanjani… hivi anavyoendelea (kufunga)tunaweza kuona anafunga mabao zaidi. Lazima ieleweke huyu ni mshambuliaji bora hapa Tanzania. Anastahili kuendelea kuwa hapa.”
Pedro pia alimtaka Dube kuamka na kufunga zaidi kwa kuwa nafasi ya kufanya hivyo anayo kutokana na ubora wa timu na hasa inavyocheza soka la kushambulia.
“Dube ukiacha kufunga ana faida kubwa sana uwanjani, Ndio maana mnaona tunaendelea kumuamini. Kitu anachotakiwa kufanya sasa ni kuendelea kufunga zaidi ili afanye makubwa hapa,” alisema kocha huyo Mreno aliyeongeza:
“Tuna timu nzuri, tuna washambuliaji wengine nao wanatakiwa kuendelea kuimarika… soka tunalocheza hapa wanatakiwa kuendelea kufunga zaidi.”