Kocha Pamba Jiji akiri mambo ni magumu

KOCHA Mkuu wa Pamba Jiji, Francis Baraza amekiri Ligi Kuu Bara msimu huu, presha ni kubwa kwa nafasi iliyopo timu hiyo, huku akitoa mapumziko kwa mastaa hadi Januari 3, mwakani.

Pamba Jiji ipo nafasi ya tatu katika msimamo baada ya kucheza mechi tisa ikikusanya pointi 16, ikishinda nne, kutoka sare nne na kupoteza mara moja.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Baraza alisema licha ya kufanya vizuri kwa kushika nafasi tatu za juu lakini presha upande wao ni kubwa, kwani wanatamani kuendelea kusalia nafasi hiyo, ila kasi ya wapinzani waliopo katika ligi hiyo wanawapa ugumu.

“Kukaa nafasi za juu sio raha kama wengine wanavyofikiria, kuna presha kubwa na unajua ukiongoza unatakiwa kuwa bora na mwendelezo mzuri wa kupata matokeo, lakini kwa namna ligi inavyocheza sio rahisi,” alisema kocha huyo raia wa Kenya aliyeongeza:

“Hili ni duru la kwanza la kujihakikishia nafasi ya kucheza ligi msimu ujao, nimekaa na wachezaji na kuwaeleza wanatakiwa kuendana na kasi ya ushindani kwa duru hili na lile lijalo ambalo litakuwa gumu zaidi.”

Baraza alisema anafurahishwa na uwezo mkubwa wa wachezaji wa kufanyia kazi kile anachowaelekeza uwanja wa mazoezi na kusisitiza ligi ni ngumu na inahitaji mbinu bora ili kuendana na ushindani uliopo.

Akizungumzia mapumziko kupisha Fainali za Afcon 2025 zinazotarajiwa kufanyika Morocco,  alisema mara baada ya suluhu na Tanzania Prisons ametoa mapumziko kwa wachezaji na kuwataka warudi Januari 3, 2026 iki kuanza maandalizi ya mechi zijazo.

“Ni kweli ni mapumziko ya muda mrefu, hii inatokana na ratiba ilivyo, huwezi kukaa na wachezaji kambini muda mrefu na hakuna mechi za mashindano, tutakaporejea tutaanzia tulipoishia na nimewaambiana nini cha kufanya wakiwa mapumziko,” alisema Baraza.

Fainali za Afcon zinatarajiwa kuanza Desemba 21 na kufikia tamati Januari 18 mwakani ikiwa ni siku tatu kabla ya kurejea kwa Ligi Kuu, Januari 21.