Muya: Dhidi ya Yanga Tumeshindwa kushikilia bomba

BAADA ya kupoteza pointi tatu dhidi ya Yanga, Kocha mkuu wa Coastal Union, Mohammed Muya amesema kipigo cha Yanga kilichangiwa na wenyewe kushindwa kushikilia bomba, japo ubora wa wachezaji wa timu pinzani umeamua mechi na kufurahia kufanikiwa kimbinu.

Coastal imekubali kipigo cha bao 1-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, iliyopigwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na kuifanya timu hiyo iliyocheza mechi nane, kusalia nafasi ya 11 baada ya kuvuna pointi tisa, ikishinda mbili, sare tatu na kupoteza tatu, lakini ikiendeleza uteja mbele ya Yanga tangu 2021.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Muya alisema mipango ya kuingia kwa kumheshimu mpinzani ilifanikiwa kwa asilimia 85, lakini ubora wa nyota wa Yanga umeamua matokeo.

“Kimbinu kwa asilimia kubwa tulifanikiwa, tulidhibiti mianya mingi ya wapinzani na nikiri mechi haikuwa bahati yetu kupata pointi tatu au hata moja kutokana na ubora wa wachezaji wa Yanga ambao ndiyo umeamua mechi,” alisema Muya na kuongeza:

“Kipindi cha kwanza Yanga walijaribu kutengeneza nafasi kupitia pembeni lakini wachezaji wetu walifika kila eneo kwa wakati kuzuia wasipenye na waliporudi waliingia na mbinu ya kupita kati pia wachezaji wangu walifika kwa wakati, isivyo bahati dakika za jioni tumepoteza, hii haikuwa nzuri kwetu ila sina wa kumlaumu.”

Muya alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa juhudi walizozionyesha, huku akiwaomba radhi mashabiki wa timu hiyo na kuwataka wasiikatie tamaa timu yao kwani bado ina nafasi ya kuwa bora mechi zijazo.