Kitambulisho tiketi ya kuingia, kutoka Chanika Mjini

Dar es Salaam. Eneo la Chanika Mwisho maarufu Chanika Mjini ambalo huwa na pilikapilika nyingi za kibiashara na usafiri wa daladala, leo Jumanne Desemba 9, 2025 lina utulivu usio wa kawaida.

Mwananchi limepita maeneo hayo ambayo hadi saa 6:00 mchana yamekuwa na ulinzi mkali wa askari wa Jeshi la Polisi, huku kukiwa na vizuizi pande zote za kuingia na kutoka.

Askari hao sambamba na wale wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baadhi wana silaha za moto na wengine wana fimbo mkononi.

Imeshuhudiwa madumu, matenga ya nyanya na meza za wafanyabiashara vikiwa vimefungwa kamba na kutumika kama vizuizi barabarani.

Vizuizi hivyo vimewekwa barabara ya kuingia na kutokea Homboza, wilayani Kisarawe, mkoani Pwani.

Vingine vimewekwa barabara ya kuelekea Mvuti, Mbagala na ile inayoelekea Katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Katika vizuizi hivyo, wanaopita wamekuwa wakionyesha vitambulisho, huku wale ambao hawakuwa navyo wanatakiwa kurudi walikotoka.

Vijiwe vya bodaboda, bajaji na daladala vimesogezwa maeneo mengine nje ya vizuizi, huku usafiri wa daladala ukiwa wa kusuasua.

Leo Jumanne Desemba 9, Watanzania wanaadhimisha Siku ya Uhuru wa Tanganyika ikiwa ni miaka 64, lakini Serikali imefuta maadhimisho ikiwataka wananchi wasio na ulazima wa kutoka kubaki nyumbani.

Juma Ramadhani, dereva wa bodaboda anayefanya shughuli zake maeneo hayo amesema abiria wanapatikana kwa shida kutokana na watu wengi kutotoka majumbani.

Kwa upande wake, Ally Kinje, anayefanya shughuli za bodaboda Zingiziwa, amesema ameamua kukaa nyumbani kusubiria wateja wanaompigia simu kwa kuwa haoni haja ya kukaa kijiweni.

“Hali ya leo siyo nzuri, nimeamua nikae nyumbani na familia, ninatoka tu pale mteja atakaponipigia simu,” amesema.

Mbali ya usafiri, maduka machache yamefunguliwa, huku baadhi ya wachuuzi wakiwataka wateja wanaokwenda dukani kuwa na vitambulisho.

Katika maeneo hayo maduka mengi huuza mikate, lakini leo Desemba 9, bidhaa hiyo imeadimika.

Mwananchi limeshuhudia watu wanaotafuta mikate wakielezwa na wachuuzi kuwa ilikwisha tangu jana Desemba 8, kwa kuwa ilinunuliwa kwa wingi.

Mfanyabiashara ambaye hakupenda kutajwa jina amesema mikate kwake ilikwisha Desemba 7 kwa kuwa ilinunuliwa kwa wingi.

Hata hivyo, bidhaa nyingine kama mchele, sukari, unga wa ngano na wa mahindi amesema upo kwa kuwa nao walijipanga mapema kuhakikisha zinakuwapo.

Sokoni walionekana wateja wachache waliokwenda kufuata mahitaji.

Amina Ally, mfanyabiashara sokoni amesema anajuta kufungua biashara kwa kuwa hakuna wateja.

Amesema kukaa hapo siku nzima ni gharama kama hujafanya biashara ina maana ni hasara kwako kwa kuwa utahitajika nauli, kula na mambo mengine.