Unguja. Kongamano la tisa la Kiswahili la kimataifa linatarajiwa kuwakutanisha wahadhiri na watafiti wa lugha kutoka mataifa mbalimbali duniani kujadili fursa za matumizi ya Kiswahili.
Kongamano hilo litafanyika siku mbili kesho na keshokutwa katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari leo Jumanne Desemba 9,2025, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma amesema kongamano hilo linalenga kutoa fursa za matumizi ya lugha hiyo inayojenga jamii yenye mshikamano na upendo.
Amesema, katika dunia ya sasa lugha hiyo haipo kwa mawasiliano pekee badala yake ni nyenzo ya kukuza elimu, uchumi, diplomasia, teknolojia na utambulisho wa mwafrika.
“Lugha ya Kiswahili inatumika kuwa ni kitega uchumi cha kuzalisha ajira kwa wadau mbalimbali,” amesema Pembe.
Ameeleza kuwa, kongamano hilo litatoa fursa ya kujadili nafasi ya Kiswahili katika sayansi na teknolojia, umuhimu wa Kiswahili katika ujenzi wa maarifa, kuiangalia kama lugha ya kazi katika jumuiya ya Afrika Mashariki na changamoto na fursa za ukuzaji wa Kiswahili katika karne ya 21.
Amefafanua kuwa, majadiliano hayo yatachangia kubuni njia mpya za kuimarisha hadhi ya Kiswahili kimataifa na kuelekeza hatua za kisera kwa lengo la kuifanya lugha hiyo kuwa chombo imara cha maendeleo ya kijamii.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza), Dk Mwanahija Ali Juma amesema washiriki wa kongamano hilo watapata nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo Zanzibar.