Mshtakiwa wa dawa za kulevya alivyotoroka Bandari ya Dar

Dara es Salaam. Mkuu wa Kitengo cha Uhalifu Mtandaoni kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Andrew Malulu, ameieleza mahakama namna alivyomkamata Kulwa Mathias (32), anayedaiwa kusafirisha bangi kutoka Tabora kwenda Zanzibar kwa kutumia boti.

Mathias alikamatwa katika Kijiji cha Solwa, wilayani Shinyanga Vijiji. Alikuwa mashineni akikoboa mpunga akarejeshwa Dar es Salaam anakodaiwa kutenda kosa la kusafirisha dawa za kulevya.

Malulu, Mkaguzi wa Jeshi la Polisi anayefanya kazi ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ametoa ushahidi jana Jumatatu, Desemba 8, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mathias na Edina Paul, wanakabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa gramu 512.50.

Wawili hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Mei 11, 2024 eneo la ukaguzi wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.

Washtakiwa wanadaiwa  walikuwa wakisafirisha dawa hizo kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kwa kutuma boti ya Zanzibar 1 zikiwa kwenye begi la kubeba mgongoni lenye rangi nyeusi na nyekundu.

Inadaiwa Mathias alikimbia na kumuacha Paul eneo la ukaguzi wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, baada ya kugundulika kuwa ndani ya begi kuna bangi.

Mathias alikamatwa Juni 13, 2024 Kijiji cha Solwa na kurejeshwa Dar es Salaam.

Akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Adolf Verandumi akishirikiana na wakili Neema Kibodya, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube, shahidi Malulu amedai Juni 12, 2024 aliitwa na mkuu wake wa kazi ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Shinyanga, aitwaye Thomas Kyondo.

“Mkuu aliniambia kuna mtuhumiwa wa dawa za kulevya anatafutwa katika Mkoa wa Shinyanga na anapatikana Kijiji cha Solwa, Shinyanga Vijiji,” amedai Malulu, shahidi wa tano wa upande wa Jamhuri.

Amesema: “Baada ya kupewa taarifa tuliondoka Shinyanga mjini saa 10:00 jioni kwenda Solwa nikiwa na wenzangu watatu, akiwemo Koplo Said.  Tulifika saa 11:00 jioni, hatukufanikiwa kumuona mshtakiwa.”

Ameeleza walilala hadi kesho yake wakiendelea kumtafuta na ilipofika saa 2:00 asubuhi walipata taarifa za intelijensia kuwa yupo mashine ya kukoboa nafaka.

“Tulimkamata na kumueleza tuhuma zinazomkabili, tuliondoka naye hadi Kituo Kikuu cha Polisi Shinyanga kwa ajili ya mahojiano,” amedai Malulu ambaye amekuwa katika kitengo hicho tangu mwaka 2014.

Ameeleza yeye ndiye alichukua maelezo ya onyo ya mshtakiwa akidai amezaliwa mwaka 1993 wilayani Magu mkoani Mwanza.

“Mshtakiwa alinieleza makazi yake ya sasa ni Zanzibar eneo la Kitopeni ambako anajihusisha na kazi ya ufyatuaji matofali, ana mke na watoto watatu,” amedai.

Amedai mshtakiwa alimwambia wamezaliwa pacha, yeye ni Kulwa na Doto yupo Tabora.

“Aliniambia hajui kusoma na kuandika, kwani baada ya kuzaliwa wazazi wake wawili walifariki dunia, yeye na wenzake walichukuliwa na shangazi yao aliyewalea hadi walipofikia hatua ya kujitegenea, hivyo hakupata nafasi ya kwenda shule,” amedai.

Malulu, ambaye majukumu yake ni kufanya uchunguzi, kukusanya ushahidi, kuwakamata na kuwahoji watuhumiwa wa makosa ya jinai na kuwafikisha mahakamani, amedai mshtakiwa alimwambia Mei 2024 alikwenda Tabora kumsalimia Doto, alipoondoka alipewa bangi apeleke Zanzibar.

“Aliniambia aliondoka Tabora kwenda Zanzibar akiwa na Edina Paul, aliyepanga kwenda kumuoa na walipofika Dar walikata tiketi mbili za boti kwa ajili ya kwenda Zanzibar,” amedai.

Amedai wakiwa eneo la ukaguzi wa mizigo, wakaguzi walibaini begi lake likiwa na majani makavu ndani, wakauliza nani mmiliki wa bagi hilo.

“Alinieleza alivyoona hivyo alitoka chumba cha ukaguzi na kukaa sehemu ya kusubiria abiria, akishuhudia kila kitu kilichokuwa kinaendelea. Baadaye alitoka nje ya chumba cha kusubiria abiria,” amedai.

Alielezwa na mshtakiwa kuwa baada ya kutoka nje alimpigia simu Doto akamweleza Paul amekamatwa, hivyo anaomba amtumie Sh100,000 za nauli ili arudi Shinyanga.

Amedai kesho yake mshtakiwa alikata tiketi akarudi Shinyanga kujipanga ili kurudi Dar es Salaam kumsaidia Paul aliyekuwa chini ya ulinzi.

Amedai mshtakiwa alimweleza ana mwaka wa tano anatumia bangi ambayo amekuwa akipewa na Doto na wakati mwingine huenda kuchukua Shinyanga.

“Mshtakiwa alinieleza hauzi bangi bali ni kwa matumizi yake, lakini mdogo wake Doto ndiye kazi yake anawauzia watu huko Tabora,” amedai.

Malulu amedai baada ya kumaliza kuandika maelezo ya mshtakiwa, alimsomea  kisha akaweka saini ya dole gumba katika maelezo hayo.

Shahidi alimtambua mshtakiwa mahakamani akaomba maelezo yapokewe na mahakama kama sehemu ya ushahidi wa upande wa Jamhuri.

Mshtakiwa alipinga kupokewa maelezo hayo akidai aliitwa kutia saini maelezo ambayo hakuandika.

“Sijaandika maelezo haya, nilitolewa mahabusu na kuambiwa kuna ndugu zangu wamekuja kuniwekea dhamana Polisi, hivyo nisaini maelezo hayo kwa kuweka dole gumba,” amedai.

Alipoulizwa alisaini vipi maelezo hayo wakati hajui kuandika na kusoma, mshtakiwa alikaa kimya.

Hakimu Makube ametoa uamuzi wa kupokea maelezo hayo akisema mshtakiwa hajaieleza mahakama anapinga kwa sababu zipi.

“Maelezo hayo yanapokewa na mahakama na kuwa kielelezo namba tano cha upande wa Jamhuri,” amesema.

Baada ya ushahidi, alihojiwa maswali ya dodoso na mshtakiwa na sehemu ya maswali ilikuwa kama ifuatavyo:

Mshtakiwa: Shahidi unadai ulinikamata mashine ya kukoboa mpunga, huko Shinyanga ni kweli?

Mshtakiwa: Wakati unanikamata ulinikuta nikiwa na nini?

Shahidi: Ulikuwa na simu ndogo.

Mshtakiwa: Hukunikuta na kitu kingine zaidi ya simu ndogo, ni kweli?

Shahidi: Nilikukuta ukiwa na simu ndogo.

Mshtakiwa: Baada ya kunikamata ulinipa haki zangu za msingi?

Shahidi: Ndiyo, nilikupa haki zako za msingi, hata hapa mahakamani nimezieleza.

Mshtakiwa: Hati ya ukamataji unayo?

Shahidi: Hapa mahakamani sijaieleta, ila ipo.

Mshtakiwa: Wakati unachukua maelezo yangu, uliita ndugu zangu?

Shahidi: Nilikupa haki zako kwa kukueleza kuwa unatakiwa uwe na ndugu zako ama wakili wako au haki ya kuandika maelezo yako mwenyewe bila kuwa na uwakilishi wowote. Ulisema upo tayari kutoa maelezo yako mweyewe kwa hiari yako bila kuwepo ndugu.

Mshtakiwa: Shahidi mahakama hii inataka kujiridhisha baada ya kunikamata na kunifikisha mahakamani, ulinipa haki zangu za msingi?

Shahidi: Nimeshajibu, uliza swali lingine.

Kesi itaendelea kusikilizwa shahidi mwingine kesho Jumatano Desemba 10, 2025.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa walifikishwa mahakamani Machi 5, 2025 na kusomewa kesi ya jinai namba 5543 ya mwaka 2025.