Morogoro. Abiria 40 wamenusurika baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Dar es Salaam kwenda wilayani Malinyi mkoani Morogoro kuteketea kwa moto katika eneo la Maseyu mkoani hapa.
Tukio hilo limetokea leo asubuhi, Desemba 9, 2025, katika kona kali ya Maseyu, Kata ya Gwata ambapo basi hilo aina ya Tata lilianza kuwaka moto na kuungua lote huku abiria wakifanikiwa kutoka wakiwa salama.
Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 9.2025 mjini hapa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amesema basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Halfan Omary, mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam, na lilikuwa limepakia abiria 40 ambao wote wameokolewa bila majeraha.
“Hili gari limeteketea kabisa, lakini tunashukuru hakuna abiria aliyejeruhiwa. Hata hivyo, mizigo na mali nyingine za abiria zilizokuwamo ndani zimeungua,” amesema Kamanda Mkama.
Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya mfumo wa umeme wa gari, ingawa uchunguzi wa kina unaendelea kubaini undani wa tatizo hilo.
Kamanda Mkama ametoa wito kwa wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya usafiri kuhakikisha magari yao yanapatiwa ukaguzi na matengenezo ya mara kwa mara, hususan yale yanayobeba abiria, ili kuepusha majanga yanayoweza kuhatarisha maisha ya watu na kuharibu mali.
