WAKATI Azam FC ikiendelea kuchekelea ushindi wa mabao 2-0 iliyopata katika mechi ya Dabi ya Mzizima dhidi ya Simba, upande mwingine ni maumivu kwa Simba hususani kocha wa muda Seleman Matola.
Matokeo hayo ni kama yamemtibulia dili kocha huyo mzawa, aliyekuwa akitajwa kama anayefaa sasa kuachiwa jumla timu hiyo, kwani kwa sasa hatma ya kusalia kikosini ipo mikononi mwa kocha mpya anayesakwa.
Mwishoni mwa wiki ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ilipokea kipigo hicho cha kwanza katika Ligi Kuu Bara, msimu huu na kutibua rekodi ya kucheza mechi mfululizi bila kupoteza, kwani ilishinda mechi nne za awali kabla ya hiyo ya tano iliyolala kwa Azam.
Ipo hivi. Inaelezwa ndani ya Simba kulikuwa na mvutano kabla ya mechi ya Azam juu ya upande mmoja uliokuwa unamtaka Matola apewe timu na ulikuwa unaonekana kushinda, lakini ghafla mambo yamebadilika kufuatia matokeo hayo ya kipigo cha Azam.
Taarifa kutoka Simba, ni kwamba, upande ambao ulikuwa unataka timu hiyo itafute kocha mpya wa kigeni, umeonekana kishinda ghafla kutokana na namna Wekundu hao walivyopoteza kimbinu uwanjani dhidi ya Azam.
Upande huo, ulikuwa unataka kuletwa kocha mpya wa kigeni ambao mchakato umeshika kasi baada ya mechi ya juzi na wale waliotaka Matola waaminiwe ni kama wameishiwa pawa.
Chanzo kutoka Simba kinasema kwa sasa mabosi wa klabu wanakimbizana kutafuta kocha mpya haraka, ili aje kuchukua nafasi ya Dimitar Pantev aliyetimuliwa wiki iliyopita baada ya timu kupoteza mechi mbili mfululizo za Kundi D ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro Atletico ya Angola na Stade Malien ya Mali.
“Tumepoteza mechi muhimu na kitu kibaya unaona namna tulianza vizuri, lakini hesabu za kiufundi ilizofanya Azam FC, ndizo zimeharibu kila kitu, sasa hapo ni ngumu kweli kuendelea kumwamini Matola, ni kijana wetu mtiifu, lakini hapa lazima tutafute kocha mwingine,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Tunatakiwa kukamilisha dili hili la kocha mpya haraka, unaona namna hali ilivyo nje, mashabiki wamekuwa wakali sana, bahati mbaya wenzetu wameshinda siku hiyo hiyo kwa tabia ya hizi klabu lazima ufanye kitu tofauti.
“Wachezaji wetu nao hatuwafurahii kwa namna wanavyocheza, tutawaangalia zaidi akija kocha mpya atakachoshauri tutafanya kama tutaona hawaleti mabadiliko.”
Chanzo hicho, kiliongeza, kuna uwezekano mkubwa kukafanyika mabadiliko zaidi katika benchi la ufundi ikiwezekana hata Matola kuondolewa kabisa, ila itategemea masharti ambayo kocha mpya atakuja nayo.”
Chanzo hicho, kiliongeza kwa kusisitiza: “Tunaweza kwenda mbali zaidi ya hapo kwa kumleta kocha mpya, unajua hizi kelele za Matola zimekuwa nyingi na huwa tunakuwa wabishi tu kumbakisha, ili kumsaidia kocha mpya anayekuja, unajua maamuzi ya kumbakisha Matola watu hawaelewi, ila hawa makocha wanakuja na kuondoka sasa ikitokea kama alivyoondoka Fadlu ina maana unakosa mtu kabisa wa kusimamia timu ndiyo msingi wa kubaki na Matola.”
Mechi ya juzi dhidi ya Azam FC ilikuwa ni ya pili tangu Matola akaimishwe ukocha mkuu, awali akishinda kwa mabao 3-0 dhidi ya Mbeya City iliyoendeleza rekodi ya kutiwahi kupoteza katika mechi za kwanza kila anapokabidhiwa timu tangu akipotua Msimbazi mwaka 2019 akitokea Polisi Tanzania.