Mgunda: Sawa tumejipata, lakini kazi ipo

KOCHA Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda amesema pamoja na nyota wake kumpa matumaini ya kufanya vizuri katika Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini amedai kukutana ugumu akiahidi kutumia mapumziko ya kupisha michuano ya Afcon 2025 ili kukiboresha zaidi kikosi hicho.

Pia, amesema yaliyotokea msimu uliopita kwa timu hiyo kuponea chupuchupu kushuka daraja hawatarajii yajirudie, akiwashukuru viongozi wao kwa kutekeleza mapendekezo ya benchi la ufundi.

Namungo haikuwa na mwanzo mzuri msimu huu kwani kati ya michezo sita ya awali ilishinda mmoja dhidi ya Tanzania Prisons 1-0, sare tatu mbele ya Pamba Jiji, JKT Tanzania na Azam FC na kupoteza mmoja kwa Simba kwa mabao 3-0.

Kwa sasa ‘Wauaji wa Kusini’ wameonekana kuimarika kwa kushinda mechi mbili mfululizo wakianza na Dodoma Jiji 2-0 na Mbeya City 1-0, na kuwaweka katika nafasi ya nne kwenye msimamo wakiwa na pointi 12 baada ya kucheza michezo minane.

Ligi Kuu Bara inasimama kwa muda kupisha fainali za Mataifa ya Afrika zinazofanyika Morocco kuanzia Desemba 21, ambapo inatarajia kurejea Januari 23 mwakani ambapo timu hiyo itashuka uwanjani kuikaribisha Coastal Union kisha kuifuata TRA United.

Mgunda ameliambia Mwanaspoti kuwa kwa sasa anaridhishwa na mwenendo wa timu hiyo kwa namna nyota wake walivyoingia kwenye mfumo wake na kwamba mwanzo ulikuwa mgumu kutokana na ushindani wa ligi.

Alisema kutokana na yaliyojitokeza msimu uliopita benchi la ufundi linaendelea kusahihisha makosa ili kuhakikisha kwamba hayajitokezi tena na wakati ligi ikisimama watakuwa na jukumu la kuboresha zaidi kikosi.

“Tunakwenda kutumia mapumziko kujisahihisha na kuboresha (upungufu) ili tunaporejea uwanjani tufanye vizuri zaidi. Niwapongeze viongozi kwa kutekeleza mapendekezo ya benchi la ufundi,” alisema Mgunda.

“Vijana wameonyesha matumaini na hatutaki yajirudie ya msimu uliopita. Tunakubali ligi imekuwa ngumu, kila timu imejipanga ndio maana tumezidiana pointi ndogo.”