MBEYA City imeshamtambulisha Mecky Maxime kuwa kocha mkuu ili kuanza kazi ya kuirudishia makali timu hiyo, lakini ametua na wawili.
Maxime anachukua nafasi ya Malale Hamsini ambaye licha ya kuanza msimu vizuri, lakini ghafla mambo yalibadilika na pande hizo mbili kukubaliana kuachana.
Taarifa za ndani kutoka Mbeya City zimelidokeza Mwanaspoti kwamba, Maxime anaweza kuanza kazi Jumatatu wiki ijayo ambapo mtu wa kwanza atakayejiunga naye ni msaidizi Nizar Khalfan ambaye alikuwa naye Dodoma Jiji msimu uliopita.
Maxime pia kabla ya kwenda Dodoma Jiji aliwahi kufanya kazi na Nizar katika iliyokuwa Ihefu kabla ya kubadilishwa jina na kuwa Singida Fountain Gate, na kwa muda walikuwa wote nje wakiwa hawana timu.
Mbali na Nizar, pia Maxime atashuka na mtaalamu mwingine ambaye ni kocha wa viungo Francis Mkanula, ambaye amekuwa naye kwa muda mrefu wakianzia Kagera Sugar, Ihefu na hata Dodoma Jiji.
Kocha huyo pia amekubaliana kubaki na kocha wa makipa, Patrick Mwangata, ambaye wanamkuta ndani ya kikosi hicho wakiwa pia wamewahi kufanya kazi pamoja katika kikosi cha Mtibwa Sugar ya Morogoro.
“Kocha Maxime anakuja na watu hao wawili. Tunataka kumpa karibu kila kitu anachotaka ili aweze kuibadilisha timu. Bado hajafika Mbeya, lakini tunaamini mpaka Jumatatu wiki ijayo atakuwa ameshafika na kuanza kazi,” kilisema chanzo kutoka Mbeya City.
“Tunaamini bado tuna timu nzuri, ukiangalia hata tulivyoanza msimu tulikuwa vizuri ghafla tu mambo yakabadilika hapa katikati. Changamoto zingine kocha akikiona kikosi atakuja kutushauri.”
Maxime ameipokea Mbeya City ikiwa katika nafasi ya 13 kati timu 16 kwenye msimamo wa ligi ikishinda mechi mbili kati ya 10 ilizocheza, huku ikipoteza sita na sare mbili. Timu hiyo imerejea Ligi Kuu Bara msimu huu ikitokea Championship ikiwa pamoja na Mtibwa Sugar.